Shughuli za uokoaji wakulima waliozingirwa na mafuriko katika eneo la mashambani kijijini Matongo wilayani Tarime
Faida za kuwepo mwekezaji mwenye uwezo, teknolojia za kisasa na mahusiano mazuri na jamii umedhihirika kutokana na Kikosi cha Dharura na Uokoaji (ERT) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara ambacho kimesaidia kuokoa watu 22 wakiwemo watoto - waliokuwa wamezingirwa na mafuriko na kukwama kwa siku mbili katika kijiji cha Matongo, wilayani Tarime.
Wananchi hao walizingirwa na maji ghafla kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kulazimika kupanda juu ya miti ili kunusuru maisha yao, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.
“Tulijitahidi kuokoa maisha yao wote waliokuwa wamezingirwa na maji na hakuna kifo wala majeruhi. Kwa hivyo, lazima tuwashukuru watu wa mgodi walifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na timu ya uokoaji ya wilaya na mkoa,” Meja Gowele aliwambia waandishi wa habari.
Alifafanua kuwa kikosi cha uokoaji kutoka mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals kilitangulia kwenye eneo la tukio mara baada ya kupata taarifa - kikiwa na boti, magari na vifaa vingine vya kisasa vya uokoaji.
Shughuli za uokoaji zilianza Jumamosi iliyopita saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni katika eneo la Mashambani lenye makambi ya wakulima na wafugaji.
“Mimi mwenyewe nilikuwepo tangu mwanzo hadi mwisho na Kamati ya Usalama, pamoja na timu za uokoaji za wilaya na mkoa zikishirikiana na mgodi ambao walitusaidia kwa kutoa vifaa vya kisasa kwa ajili ya uokoaji. Kwa hivyo, tuna kila sababu ya kuwashukuru watu wa mgodi kwa kazi waliyofanya,” alisema Meja Gowele.
Baada ya kuokolewa, wananchi hao walipatiwa huduma ya kwanza na kusaidiwa kurejea kwenye makazi yao katika vijiji mbalimbali wilayani Tarime.
“Baada ya kuwatoa tuliwacheki kuona kama wanahitaji matibabu lakini wengi walikuwa wana njaa na niliagiza wakapata uji na maji,” alisema Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, alimshukuru Mkuu wa Wilaya, Gowele na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuchukua hatua za haraka kuokoa watu hao baada ya kuwapa taarifa za tukio hilo.
“Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Mgodi wa Barrick North Mara kwa namna walivyopokea jambo hii na kufika kwa muda muafaka, hii inadhirisha wazi kuwa mahusinao yetu na Barrick ni mazuri,” alisema Ryoba mara baada ya shughulli za uokoaji kukamilika.
Alizishukuru pia timu za uokoaji za wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa kujitokeza kushiriki kuokoa maisha ya wananchi hao bila kukata tamaa.
Shughuli za uokoaji wakulima waliozingirwa na mafuriko katika eneo la mashambani kijijini Matongo wilayani Tarime














