
Dunia ya sasa haina nafasi kwa taifa linalojitenga, na wakati wanaharakati wa mtandaoni wakipoteza muda kuiombea mabaya Tanzania, Serikali ya Awamu ya Sita imejibu kwa vitendo vikubwa vinavyothibitisha kuwa harakati hizo ni za kipuuzi na hazina nafasi mbele ya wenye akili wanaozungumza na Serikali.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ameziamsha hisia za kimataifa jijini Dar es Salaam kwa kutoa hakikisho la ushirikiano usioyumba na mataifa ya Italia na Canada, akisisitiza kuwa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania si kisiwa bali ni kitovu cha uwekezaji kinacholenga kufuta umaskini.
Ushirikiano na Italia pekee tayari umemwaga zaidi ya Euro milioni 509—zaidi ya Shilingi trilioni 1.4—katika miradi ya kimkakati iliyogusa elimu ya ufundi kama vyuo vya Arusha, MUST na DIT, huku ikiboresha mifumo ya takwimu na usajili wa vizazi nchi nzima.
Huu si wakati wa maneno matupu bali ni wakati wa miradi ya kimkakati, ambapo Italia imetakiwa kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo kama kahawa, huku kampuni zake zikitambuliwa kama walipakodi wakubwa nchini.
Moto huo wa maendeleo umechochewa zaidi na Serikali ya Canada, ambapo Balozi Emily Burns amekiri wazi kuwa wawekezaji wa nchi hiyo wanamiminika Tanzania kutokana na mazingira bora ya biashara yaliyowekwa na Rais Samia.
Serikali imejipanga kusafisha njia zaidi kwa kufanyia kazi mikataba ya kuzuia kodi mara mbili, ikilenga sekta za afya, kilimo, na ulinzi wa jamii ili kuhakikisha ustawi wa kila Mtanzania.
Hatua hizi za kijasiri na kukubalika kwa Tanzania katika medani za kimataifa ni dhihirisho tosha kuwa jitihada za kuichafua nchi zimeshindwa, na badala yake, taifa linasonga mbele kwa kasi ya ajabu kuelekea maendeleo endelevu na utajiri wa kijamii na kiuchumi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464