
Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutengeneza ajira zenye staha kwa vijana yameanza kudhihirika kwa vitendo mkoani Dodoma, huku Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (Building a Better Tomorrow - BBT) ikitajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi na silaha dhidi ya umaskini wa kipato.
Hayo yamebainishwa na vijana wanufaika wa programu hiyo kutoka kikundi cha Wanyeusi, kilichopo Kijiji cha Manchali 'A' wilayani Chamwino. Vijana hao wameeleza kuwa juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta mapinduzi makubwa yanayowahakikishia ajira ya kudumu mashambani, tofauti na dhana ya zamani ya kusubiri kazi za maofisini pekee.
Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia BBT ni uwezo wa vijana hao kubadili mfumo wa kilimo. Badala ya kutegemea msimu mmoja wa mvua, sasa wanafanya kilimo cha biashara kwa misimu minne (4) kwa mwaka. Hatua hii imetafsiriwa na wataalamu wa uchumi kama hatua kubwa ya kuelekea kwenye ajira ya uhakika na yenye tija (Full-time Employment).
"Mpango huu umefungua ukurasa mpya wa kilimo cha kisasa. Hatutegemei tena mvua, bali teknolojia. Hii imetupa uhakika wa mavuno na kipato cha kila mwezi, jambo linalotufanya tujivunie kuwa wakulima," walisema viongozi wa kikundi hicho.
Ili kuhakikisha vijana hao hawakwami, Serikali kupitia BBT imewekeza katika miundombinu ya gharama kubwa na ya kisasa katika eneo la mradi ikiwemo ardhi ya uhakika huku wananchi wamefaidika na ugawaji wa ekari 20 za kilimo kwa kikundi hicho.
Aidha hatua nyingine ni kuwezesha maji na nishati: Eneo hilo limechimbiwa kisima kirefu cha mita 160, ujenzi wa bwawa la lita 8,050, na kuunganishiwa umeme kwa ajili ya kuendesha mitambo. Pia kumeingizwa teknolojia ya Umwagiliaji: Kufungiwa mifumo ya kisasa ya umwagiliaji (drip irrigation) inayohudumia eneo lote, hivyo kupunguza nguvu kazi ya kizamani na kuongeza ufanisi.
Wakati akizindua programu hii, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza azma yake ya kuwahamasisha vijana na wanawake kujikita katika kilimo biashara ili kuongeza uzalishaji na kupata ajira zenye heshima.
Mafanikio yanayoonekana Manchali 'A' ni uthibitisho tosha kuwa serikali imefanikiwa kutengeneza mnyororo wa thamani ambao si tu unazalisha chakula, bali unatengeneza matajiri wapya vijana (Agri-preneurs). Hii ni ishara kuwa mkakati wa serikali wa kupeleka ajira kwa vijana vijijini na maeneo ya uzalishaji unafanya kazi kwa asilimia mia moja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464