` RAS HAMDUNI AZINDUA KAMPENI YA UTOAJI CHANJO YA POLIO KWA WATOTO SHINYANGA

WANDAMAN HOTEL

RAS HAMDUNI AZINDUA KAMPENI YA UTOAJI CHANJO YA POLIO KWA WATOTO SHINYANGA

 

RAS HAMDUNI AZINDUA KAMPENI YA UTOAJI CHANJO YA POLIO KWA WATOTO SHINYANGA

******
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni amezindua rasmi kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio kwa watoto chini ya miaka 10 yenye lengo la kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya ugonjwa huu na kuzuia maambukizi kutokea.

Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa leo Machi 24, 2026 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mapinduzi B, RAS Hamduni ametoa wito kwa walimu, wataalamu wa afya, viongozi wa dini na kisiasa kuendelea kuwahamasisha wazazi kushiriki ipasavyo kwa kuwaleta watoto kupewa chanjo ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo na kuzuia ulemavu.
“Niwasihi walimu, wataalamu wa afya na viongozi wa dini na kisiasa kuwahamasisha wazazi na walezi kuwaleta watoto wao katika vituo vilivyoainishwa kwa ajili ya zoezi la utoaji chanjo kwa watoto ili kuwalinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu” amesema Hamduni.

Aidha ameeleza kuwa kampeni hii inafanyika ili kuzuia maambukizi kama kinga ya awali na zoezi hili litadumu kwa siku 4 likitarajiwa kuwafikia watoto 781,186 ndani ya Mkoa wa Shinyanga huku timu ya wataalamu 1400 tayari imeandaliwa ili kufanikisha zoezi hili muhimu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Yudas Ndungile, amesema kuwa Serikali imeanzisha kampeni hiyo mara baada ya kubainika kwa vimelea vya ugonjwa Polio katika maji taka jijini Mwanza, hali inayoongeza hatari ya maambukizi kwa watoto.

Naye Mratibu wa Miradi ya Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Bi. Dina Atinda, amesema chanjo hiyo ni salama ikiwa tayari imefanyiwa vipimo na kuthibitishwa ubora wake huku akitoa wito kwa wazazi kuwaeleza wengine kuhusu umuhimu wa kuwaruhusu na kuwaleta watoto wao kupata chanjo hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Bi. Anne Shuma, amesema kampeni hiyo ya utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka 10 itatotelewa katika maeneo mbalimbali kam vile Shuleni. Sokoni, Vituo vya kulea watoto mchana, nyumba kwa nyumba na maeneo mengine ambayo wanapatikana watoto.

Nao wawakilishi wa wazazi walioshiriki kuwaleta watoto kupata chanjo hiyo ambao ni Frank Chingula na John John, wameishukuru sana Serikali kwa kuandaa kampeni hii muhimu itakayowakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Polio huku wakitoa wito kwa wazazi wengine kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalamu na kuwaleta watoto wao ili wapate chanjo na kuwa na afya njema kwani chanjo hii ni salama kwa watoto.

Kampeni hii ambayo inafanyika kuanzia leo Machi 24 – 27, 2026 ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya utoaji chanjo kwa watoto ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Polio katika mikoa 7 ambayo ni Shinyanga, Mwanza, Mara, Tabora, Simiyu, Geita na Singida, huku awamu ya pili ya utoaji chanjo ikitarajiwa kuanza Mei 7 – 10, 2026.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464