` MISA TANZANIA WAFANYA UTALII WA NDANI IRINGA KUTANGAZA VIVUTIO

WANDAMAN HOTEL

MISA TANZANIA WAFANYA UTALII WA NDANI IRINGA KUTANGAZA VIVUTIO


MISA TANZANIA WAFANYA UTALII WA NDANI IRINGA KUTANGAZA VIVUTIO

Na Marco Maduhu, IRINGA

Wahariri ,waandishi wa habari na wadau wa habari wanaoshiriki kongamano la Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA Tanzania) wamepata fursa ya kufanya utalii wa ndani mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Ziara hiyo imefanyika leo Machi 18, 2026 ikiwa ni sehemu ya siku ya pili ya kongamano la MISA TAN Summit 2026, ambapo washiriki walitembelea hifadhi mbalimbali kujionea vivutio vya utalii ikiwamo Makumbusho ya Chifu Mkwawa.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo Mwenyekiti wa Misa Tanzania Edwin Soko, amesema, lengo ni kuwafanya waandishi wa habari kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii wa ndani, kwa kutumia kalamu na vyombo vya habari kuhamasisha Watanzania kutembelea maeneo ya vivutio hivyo.

Amesema Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye fursa kubwa za utalii, zikiwemo hifadhi za taifa, mandhari ya kuvutia na urithi wa kihistoria, hivyo kuna umuhimu wa vyombo vya habari kusaidia kuvitangaza ili kuchochea uchumi wa eneo hilo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza jana wakati wa kufungua Kongamanio hilo, amesema Iringa ni kitovu cha utalii katika Kanda ya Kusini ikiwa na vivutio vikubwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Udzungwa, pamoja na maeneo ya kihistoria kama Isimila na Kalenga shamba la miti "Sao Hill."
Kwa upande wao washiriki, wameeleza kuwa ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu rasilimali za utalii zilizopo nchini, huku wakiahidi kuandika na kurusha habari zitakazohamasisha jamii kushiriki utalii wa ndani.

Kongamano la MISA TAN Summit 2026 limewakutanisha wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini, likiwa na lengo la kujadili fursa za maendeleo pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuzitangaza.

Hatua ya MISA Tanzania kuunganisha kongamano na utalii wa ndani ni kuhamasisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii na kwamba sekta ya utalii ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Taifa.

Vitutio vya utalii walivyotembelea ni Iringa Boma, Gangolonga, Kihesa, Kilolo, Kalenga kwenye makumbusho ya Chifu Mkwawa, Isimila, Sao Hill kwenye shamba la Miti na kisha kupanda miti kwa kuweka alama pamoja na chuo cha mafunzo ya misitu na viwanda vya misitu FWITC .
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464