` MISA TANZANIA KUPEWA ARDHI KUJENGA KITUO CHA TAARIFA KWA JAMII IRINGA

WANDAMAN HOTEL

MISA TANZANIA KUPEWA ARDHI KUJENGA KITUO CHA TAARIFA KWA JAMII IRINGA


MISA TANZANIA KUPEWA ARDHI KUJENGA KITUO CHA TAARIFA KWA JAMII IRINGA

Na Marco Maduhu, IRINGA

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James ametoa maagizo ya kupatiwa ardhi Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika Misa Tanzania, kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa kituo cha taarifa kwa jamii (Community Telecentre) kitakacholenga kusaidia jamii kupata taarifa muhimu za maendeleo.
Ametoa agizo hilo wakati akifungua kongamano la wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari (Misa Tan Summit 2026) lenye kauli mbiu isemayo Iringa imara, tutaijenga kwa umoja na uwajibikaji.

Awali Mwenyekiti wa Misa Tanzania Edwini Soko, akisoma taarifa ya taasisi hiyo kwa mkuu wa mkoa, alisema mbali na kongamano hilo, wana mpango wa kuanzisha Kituo cha Taarifa kwa Jamii (Community Telecentre) kitakacholenga kusaidia jamii kupata taarifa muhimu za maendeleo.
Amesema kituo hicho kitatoa taarifa muhimu kwa jamii kuhusu bei za mazao na masoko, fursa za biashara na uwekezaji, teknolojia na mbinu bora za uzalishaji, elimu ya kidigitali na mawasiliano.

Amsema mpango huo unalenga kuhudumia zaidi mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Songwe, na kwamba changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa ni eneo au kiwanja cha kuanzisha kituo hicho.
“Kwa heshima kubwa tunakuomba ndugu Mgeni Rasmi, kama itawezekana kwa uongozi wa Mkoa wako kutupatia eneo hapa Iringa ili tuweze kujenga kituo hicho kwa ufadhili wa washirika wetu kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ili kusaidia jamii kupata taarifa muhumi za maendeleo,” amesema Soko.

Aidha, amesema umuhimu wa kongamano hilo, ni kukuza ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya habari na wadau wa maendeleo, kutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu mpya za uandishi wa habari kati ya wahariri na waandishi wa habari, kuimarisha uandishi wa habari unaolenga suluhisho kwa changamoto za jamii, kutangaza fursa za uwekezaji, utalii na maendeleo zilizopo katika Mkoa wa Iringa.

kuchochea mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, hususan katika kuwahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo.
“Misa Tanzania imetambua juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wako katika kuendeleza Mkoa wa Iringa, kupitia kauli mbiu ya “Iringa *Imara Itajengwa kwa Umoja na Uwajibikaji.* ” Kauli mbiu hii inaendana na dhamira ya vyombo vya habari ya kujenga jamii inayowajibika na inayoshiriki kikamilifu katika maendeleo yake,” amesema Soko.

Ameongeza” kwa kutambua juhudi hizo, wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wameamua kuja Iringa ili kujifunza, kuona na pia kusaidia kutangaza fursa zilizopo hapa mkoani kwako,”.
Soko ameleza kuwa mafanikio ya maendeleo yanayofanyika mkoani Iringa kwamba, kupitia kalamu na sauti za wanahabari kuwa fursa za Iringa zitaweza kufika kwa wananchi wengi zaidi ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James, amesema Mkoa huo upo tayari kutoa aridhi kwa ajili ya kujengwa kituo hicho kwa maslahi mapana ya wananchi.

Aidha, amesema Mkoa wa Iringa wanajivunia kuwa mwenyeji wa Mkutano huo na kwamba uwepo wa wahariri na waandishi wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni ishara ya umuhimu wa sekta ya habari katika kujenga jamii yenye uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhabarisha umma, kuelimisha jamii pamoja na kuchochea mjadala wa maendeleo, huku akibainisha kuwa kupitia kalamu zao wana nafasi ya kuathiri fikra na mwelekeo wa jamii.

“Ni heshima kubwa kwa Mkoa wetu kuwapokea wataalamu wa sekta hii muhimu. Tunawaomba muwe mabalozi wa kuitangaza Iringa ili kuvutia wawekezaji na watalii,” James.
Akitoa maelezo kuhusu Mkoa huo, alisema Iringa inaendelea kukua kiuchumi ambapo pato la Mkoa limeongezeka kutoka Sh trilioni 4.5 mwaka 2020 hadi trilioni 6.3 mwaka 2024, huku sekta ya kilimo ikiendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi kwa kuchangia zaidi ya asilimia 85.

Alisema Mkoa huo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula nchini, ukiwa na mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, viazi, mpunga na maharage, pamoja na kuwa na fursa kubwa ya kilimo cha umwagiliaji.
Aidha, alisema sekta ya mifugo imeendelea kukua ambapo uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa kiasi kikubwa, hali inayofungua fursa za uwekezaji katika viwanda vya maziwa.

Kuhusu utalii, alisema Iringa ni kitovu cha utalii katika Kanda ya Kusini ikiwa na vivutio vikubwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Udzungwa, pamoja na maeneo ya kihistoria kama Isimila na Kalenga.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, maji, umeme, afya na elimu ili kuboresha maisha ya wananchi na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

Katika hatua nyingine, alisema Mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda vya usindikaji wa mazao, hoteli za kitalii, pamoja na huduma za afya na elimu.

Amesisitiza kuwa kupitia mkutano huo, wanatarajia kuona mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuitangaza Iringa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mkutano huo alisema uwepo wa mkutano huo ni fursa kwa waandishi wa habari kujadili masuala muhimu ya sekta hiyo pamoja na kubadilishana uzoefu.

Katika Kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Iringa alipewa Tuzo ya Uongozi bora na Misa Tanzania.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza.
Mwenyekiti wa Misa Tanzania Edwin Soko akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Benjamini Sitta akizungumza.









Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza na viongozi wa Misa Tanzania.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464