Na Marco Maduhu, IRINGA
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia mpango wa hifadhi Scheme, umeanza kuwafikia watu waliojiajiri kwa kuwawezesha kuweka akiba kidogo kidogo na kunufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo ya uzeeni, matibabu, misiba na uzazi.
Akizungumza Machi 17, 2026 katika kongamano la Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA Tanzania) lililowakutanisha wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari, mwakilishi wa NSSF chini ya mpango huo, Elizabeth Mwankanye, amesema mfuko huo sasa umeelekeza nguvu kwa makundi maalum ya waliojiajiri kama waendesha bodaboda, mama lishe, machinga na wafanyabiashara wadogo.
Amesema awali NSSF ilionekana kuwa ni ya watu walioajiriwa pekee, lakini sasa wamepanua wigo kwa kuwafikia waliojiajiri, ambapo hadi sasa wamefanikiwa kusajili vikundi 2,148 vyenye jumla ya wanachama 5,632.
“Tunawafikia moja kwa moja kwa kutembelea vikundi vyao na tunaendelea kutoa elimu ili waweze kujenga utamaduni wa kuweka akiba,” amesema Mwankanye.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema mafanikio ya maendeleo ya mkoa huo yanachangiwa na sera rafiki za ukusanyaji mapato ambazo haziwakwamishi wafanyabiashara.
Amesema mbinu hiyo imeongeza hiari ya ulipaji kodi na kuchochea ukuaji wa viwanda pamoja na pato la mkoa, huku akibainisha kuwa kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu ni asilimia 2.4 kwa mwaka.
“Tumefanya ukusanyaji wa kodi usiwe kikwazo kwa wafanyabiashara, hali ambayo imewafanya walipakodi kulipa kwa hiari na kuongeza mapato ya mkoa,” amesema James.
Naye Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kongamano hilo linalenga kuimarisha uhusiano kati ya waandishi wa habari na wadau muhimu wakiwemo serikali.
Amesema vyombo vya habari vina jukumu la kujenga jamii kwa kutoa taarifa sahihi na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa Benedict Wella akizungumza.
Afisa wa NSSF kupitia mpango wa hifadhi Scheme Elizabeth Mwankanye akielezea mpango huo wa kuwafikia watu waliojiajiri.
Mwenyekiti wa Misa Tanzania Edwin Soko akizungumza.
Meneja wa NSSF Iringa Benedick Wella (kulia) akipewa cheti cha pongeza kwa kuwezesha Kongamano hilo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464