` TRC KUTUMIA ENEO LA WFP ISAKA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MIZIGO BANDARI YA DAR ES SALAAM

WANDAMAN HOTEL

TRC KUTUMIA ENEO LA WFP ISAKA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MIZIGO BANDARI YA DAR ES SALAAM

TRC KUTUMIA ENEO LA WFP ISAKA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MIZIGO BANDARI YA DAR ES SALAAM

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limekabidhiwa eneo lililokuwa likimilikiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), katika eneo la Isaka Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kwa ajili ya kulitumia kama kituo cha kushusha mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam kwa kuisafirisha kupitia reli hadi Isaka.

Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ili kuongeza ufanisi wa ubebaji wa mizigo na kuisambaza kwa wakati.
Makabidhiano ya eneo hilo yamefanyika Machi 7, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, akizungumza kwenye makabidhiano ya eneo hilo, amesema wanafarijika TRC, kwa kuamua kulitumia kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo, sababu mkoa huo una makongani ya uwekezaji, na kwamba utasaidia wawekezaji kusafirisha mizigo yao kwa wakati na kurahisha ufanyaji wa biashara.
“Mkoa wa Shinyanga tumefurahi na kufarijika sana na ujio wa TRC kulitumia eneo la WFP, sababu tuna kongani la uwekezaji, na unapozungumzia kongani, wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza, moja kati ya hesabu yao ya haraka sana ni namna ya usafirishaji wa mizigo yao, hivyo suluhu imepatikana, na tunaita wawekezaji zaidi waje kuwekeza Shinyanga,”amesema Mhita.

Amesema kuwa, eneo hilo awali lilikuwa likitumiwa na WFP kwa ajili ya miundombinu ya kuhifadhi chakula, na kupeleka kwenye maeneo yenye uhitaji, na kwamba moja kati ya mashirika ambayo wao wanayaamini ni TRC, hivyo anaamini wanakwenda kuwekeza kwenye eneo ambalo wanalifahamu vizuri.
Ametoa Rai kwa TRC, kwamba eneo hilo la WFP walifanyie maendeleo makubwa, na kuleta matokeo chanya kiuchumi katika Mkoa huo wa Shinyanga.

Aidha, amesema, moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kutengeneza fursa za kiuchumi kwa wananchi, na kwamba uwekezaji huo ukitarajiwa kuchochea ajira za muda mfupi na muda mrefu pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha.
Amesema uwekezaji huo wa TRC, una kwenda pia kuongeza mzunguko wa fedha, na kutoa wito kwa wadau, wachangamkie fursa za kiuchumi, ikiwamo kujenga nyumba za wageni na hoteli sababu kutakuwa na muingiliano wa watu wengi.

Mbunge wa Msalala Mabula Magangila, ameishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati katika Kata ya Isaka, akisema miradi hiyo inafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mhandisi Machibya Shiwa, amesema eneo la Isaka kama TRC ni moja ya maeneo ya kimkakati, kwamba reli zote mbili zinapoanzia bandari ya Dar es salaam, ni lazima iwe na sehemu ya kushusha mizigo, na eneo hilo ni muhimu sababu nivirahisi kwa usafirishaji wa mizigo katika nchi za Uganda, Kongo, Rwanda na Burundi.

Amesema kwamba, eneo hilo la WFP palijengwa miundombinu, kwa ajili ya kuchukua mizigo na kuipeleka kwenye maeneo ambayo yalikuwa yameathirika na vita kama Rwanda, Burundi, DRC na maeneo ya Sudani Kusini.
Amesema, eneo hilo la WFP litatumika kuipungumzia mizigo Bandari ya Dar es salaam,na kuileta Isaka kupitia Reli yetu. ili kuongeza ufanisi wa ubebaji wa mizigo.

“Hiki tunachokifanya Mkuu wa Mkoa ni mkakati wa muda mfupi, ni kuisaidia Bandari ya Dar es salaam kuchukua mzigo kuleta Isaka, sababu sasa hivi kuingia Bandari ya Dar es salaam kunachangamoto kubwa,” amesema Mhandisi Shiwa.

Ameongeza kuwa katika mkakati wa muda mrefu, TRC inapanga kujenga kituo cha reli ya kisasa ya SGR katika eneo la Isaka kwa ajili ya kuiogezea uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, na kwamba wafanyabiashara wengine watakuwa wakiagiza mizigo yao moja kwa moja katika Bandari Kavu ya Isaka badala ya Dar es Salaam.
Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, amesema eneo hilo la WFP lina ukubwa wa takribani hekta saba na lilikuwa likitumika kusambaza chakula katika kambi za wakimbizi katika nchi za DRC, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1996 na kujengwa maghala makubwa ya kuhifadhi chakula pamoja na nyumba za watumishi.

Lyamongi ameongeza kuwa eneo hilo pia lina miundombinu ya reli inayoruhusu mabehewa kuingia moja kwa moja katika maghala kwa ajili ya kushusha mizigo kwa urahisi.

Amesema kijiografia eneo hilo liko katikati ya ukanda wa Kaskazini na linaweza kurahisisha usambazaji wa mizigo na mazao kwenda katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Kagera, Shinyanga na Mara pamoja na nchi jirani kama Kenya kupitia eneo la Kisumu.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka TRC Jaffer Machano akizungumza.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mhandisi Machiya Shiwa akizungumza.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga David Lyamongi akizungumza.
Mbunge wa Msalala Mabula Magangila akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464