RAFIKI SDO WATAMBULISHA MRADI WA MKUA WILAYANI KISHAPU, KULINDA HAKI ZA WATOTO
Na Marco Maduhu, KISHAPU
Shirika la Rafiki Social Development Organization (Rafiki SDO) limetambulisha mradi wa MKUA wilayani Kishapu, utakaolenga kuwawezesha watoto kuimarisha mabaraza yao na kuanzisha madawati ya watoto shuleni, ili kujadili ustawi wao na kutatua changamoto zinazowakabili, ili kulinda haki za watoto na kuimarisha ustawi wao.
Mradi huo umetambulishwa leo Machi 5, 2026 kwa maafisa wa Halmashauri wanaohusika moja kwa moja na masuala ya watoto, akiwamo Afisa Maendeleo ya Jamii, Afisa Mipango, Mratibu wa Dawati la Watoto pamoja na Maafisa Elimu wa shule za msingi na sekondari.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng’ong’a, akitambulisha mradi huo, amesema ni wa miaka mitatu kuanzia Januari 2026 hadi Desemba 2028, ukifadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Save the Children.
Amesema mradi huo unalenga kuchangia kuziwezesha asasi za kiraia, ikiwamo watoto wenyewe, kukabiliana na changamoto za nafasi finyu ya kiraia, na kuimarisha uwezo wao wa kuwawajibisha wenye dhamana katika kutekeleza haki za watoto.
“Mradi huu utajikita zaidi katika kuimarisha mabaraza ya watoto ili kuwapa nafasi ya kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wao, ikiwamo elimu, malezi, makuzi pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika jamii,” amesema Ng’ong’a.
Amesema kupitia mabaraza hayo ya watoto ,itasaidia kukutana nao na kusikia changamoto ambazo huwakabili kutoka kwao, na hata kusababisha baadhi yao kuingia mitaani, kuwa watoro shuleni na wengine kuacha masomo.
Ng’ong’a ameongeza kuwa kuanzishwa kwa madawati ya watoto shuleni kutasaidia kushughulikia matatizo yao mapema kwa kutafuta suluhu ndani ya mazingira ya shule, badala ya matatizo hayo kufika nje ya mfumo wa shule.
“Madawati haya yatasaidia hata mzazi kuitwa shuleni ili kujadili changamoto zinazomkabili mtoto na kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na uongozi wa shule,” amesema Ng’ong’a.
Ameleza kuwa katika mradi huo, pia watashirikiana na asasi za kiraia au vikundi vya kijamii, vinavyofanya kazi za watoto, ili kuunganisha nguvu ya pamoja kuutekeleza.
Ameongeza, wao kama wadau wa maendeleo, wamejielekeza kushirikiana na serikali, kwa kuhakikisha sheria za watoto zinatekelezwa na kutimiziwa mahitaji yao, kwa kuimarisha mifumo ya utawala na kulinda haki za watoto.
Aidha, amesema mradi huo watautekeleza katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga, ambazo ni Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ushetu, Msalala, Kishapu na Manispaa ya Kahama.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Abednego Madole, amesema miradi inayolenga watoto ni muhimu, kwa kuwa inawapa nafasi ya kupaza sauti na kueleza changamoto zinazowakabili ili zipatiwe ufumbuzi.
Amesema, serikali imeupokea mradi huo, na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO Gerald Ng'ong'a akitambulisha mradi wa MKUA wilayani Kishapu.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Abednego Madole akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464