.jpg)
Katika hali inayozidi kuonesha kuwa utulivu wa nchi ndio mbolea ya ukuzaji wa kipato, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupiga hatua kubwa katika kujenga uchumi jumuishi unaowabeba wanawake na vijana.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 28, 2026, amebainisha kuwa mafanikio yote ya kiuchumi yanayoshuhudiwa sasa ni matunda ya mazingira ya amani na utulivu yaliyopo nchini.
Bila amani, jitihada za kisera kama kutenga asilimia 30 ya zabuni za serikali kwa makundi maalumu zisingeweza kutekelezeka, kwani biashara huhitaji utulivu ili kuchanua na kutoa ajira kwa jamii.
Msisitizo huo wa amani umedhihirika zaidi kupitia takwimu za kusisimua ambapo katika kipindi cha miaka minne tu, wanawake na vijana wamefanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 9 katika Soko Huru la Bara la Afrika.
Waziri Kapinga amesisitiza kuwa mafanikio haya hayakuja kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya uongozi mahiri wa Rais Samia ambaye tangu mwaka 2022 amekuwa kinara wa ushirikishwaji wa makundi haya kimataifa.
Ni wazi kuwa soko huru linahitaji nchi zenye amani ili kuruhusu bidhaa na mitaji kutembea bila hofu, jambo ambalo Tanzania imelishika kwa mikono miwili na kugeuka kuwa shamba la fursa kwa wajasiriamali.
Katika kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), serikali imeweka wazi kuwa imetenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana ili kuchochea zaidi kasi ya kujiajiri.
Rais wa TWCC, CPA Mercy Sila, amempongeza Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya biashara na kufungua madirisha ya mitaji kupitia benki na mifuko ya uwezesheshaji.
Maboresho haya ya kiuchumi yanategemea sana mnyororo wa amani, kwani mfanyabiashara anahitaji uhakika wa usalama wa mtaji wake na soko ili aweze kukua kutoka ujasiriamali mdogo kuelekea kumiliki viwanda vikubwa.
Ujumbe mkuu katika sherehe hizo za ugawaji wa tuzo za viwanda na biashara ulikuwa ni kuwakumbusha Watanzania kuwa uchumi imara unajengwa juu ya misingi ya umoja na mshikamano.
Waziri Kapinga amewataka wanawake na vijana kuendelea kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya nchi kwa sababu ndiyo injini inayofanya mipango ya serikali, ikiwemo uwezeshaji wa kiuchumi, iwe na tija. Kwa kuimarisha uchumi wa mwanamke, taifa linajenga jamii yenye ustahimilivu na amani ya kudumu, kwani tumbo lililoshiba na mfuko uliopata fursa ni kinga tosha dhidi ya migogoro na sintofahamu katika jamii
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464