
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka wimbi la kusikitisha la wasichana wa Kitanzania wanaokumbana na madhila mazito baada ya kusafirishwa kwenda mataifa ya kigeni kufanya kazi za ndani kwa kutumia njia zisizo rasmi, maarufu kama ‘njia za panya’.
Maumivu wanayoyapata vijana hawa, ikiwemo kulazimishwa kufanya kazi ngumu na wakati mwingine kuingizwa kwenye biashara haramu ya ngono, ni kilio kinachopaswa kusikika na kila mzazi na kijana anayetafuta fursa nje ya mipaka ya nchi.Mkurugenzi wa Upelelezi wa Kikosi cha Ulinzi wa Mtoto dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu, SP Geofrey Gaudiozi, ametoa onyo kali akibainisha kuwa wasichana wengi hurubuniwa kwa ahadi hewa za mishahara mikubwa na maisha ya kifahari.
Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba wanapofika nchi za ugenini, hukutana na mazingira ya utumwa mamboleo ambapo hunyang’anywa pasipoti na kushindwa kupata msaada wowote wa kisheria kwa sababu hawakusajiliwa kwenye mifumo rasmi ya serikali.
Kutokana na changamoto hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa njia pekee ya uhakika ya kupata ajira za nje ni kupitia mifumo halali inayotambuliwa na serikali.
Kampeni ya ofisi hii inalenga si tu kumpatia kijana kazi, bali kuhakikisha usalama wake mahali pa kazi (Occupational Safety and Health). Serikali imeweka utaratibu wa kusimamia mawakala wa ajira ili kuhakikisha mikataba ya kazi inazingatia utu, haki, na inatoa ulinzi kwa Mtanzania anapokuwa ugenini.
Ni muhimu kwa vijana wetu kuelewa kuwa kutumia njia zisizo rasmi ni kujiweka rehani mikononi mwa walanguzi wa binadamu ambao hawajali maisha ya mtu bali faida yao binafsi.
Ofisi ya Waziri Mkuu imeweka wazi kuwa kila kijana anayetafuta fursa nje ya nchi anapaswa kupita katika mamlaka husika ambazo zina uwezo wa kufuatilia hali ya mfanyakazi, kuhakikisha anapata stahiki zake, na kutoa msaada wa haraka kupitia balozi zetu pindi matatizo yanapojitokeza.
Mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu yatafanikiwa pale tu wananchi watakapoamua kutumia mifumo rasmi na kutoa taarifa za mawakala matapeli.
Usalama kazini huanzia kwenye mkataba halali na mfumo unaotambulika na serikali; usikubali kurubuniwa, linda utu wako kwa kufuata utaratibu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464