` ZIWA NYASA LAFUNGULIWA KITALII: BOTI YA KISASA YA 'LUNDO ISLAND TOURS' YAZINDULIWA

ZIWA NYASA LAFUNGULIWA KITALII: BOTI YA KISASA YA 'LUNDO ISLAND TOURS' YAZINDULIWA

WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma, imetajwa kuwa kitovu kipya cha utalii nchini kutokana na kusheheni vivutio vya kipekee vikiwemo visiwa vya kuvutia, fukwe zenye mchanga wa rangi mbalimbali na aina zaidi ya 400 za samaki wa mapambo ambao hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Katika juhudi za kufungua fursa hizo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas, amezindua boti mpya na ya kisasa ya kitalii iitwayo ‘Lundo Island Tours’. Boti hiyo yenye thamani ya Shilingi milioni 200, imenunuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa lengo la kuchochea utalii katika visiwa vya Lundo na Mbamba Bay.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Februari 15, 2026, Abbas amesema hatua hiyo ni sehemu ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya utalii kwenye Ukanda wa Kusini. Amewataka viongozi na jamii kushirikiana kutunza miundombinu hiyo na bayoanuai zilizopo ili kuendelea kuvutia watafiti na watalii wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa TAWA Kanda ya Kusini Mashariki, Khadija Malongo, amebainisha kuwa maboresho ya miundombinu tangu mwaka 2023 yamesaidia kuongeza idadi ya watalii hadi Desemba 2025 kufikia 752 . Amesema ujio wa boti hiyo utahakikisha watalii wanapata huduma bora na za uhakika wanapotembelea visiwa hivyo vyenye historia ya kipekee.

Mbali na uzuri wa asili, Wilaya ya Nyasa ina utajiri wa mambokale na historia. Kisiwa cha Lundo kinakumbukwa kama maficho wakati wa Vita ya Majimaji (1905-1907), huku kijiji cha Mbamba Bay kikiwa na nyumba ya kihistoria ambapo Mwalimu Julius Nyerere alilala mwaka 1956 wakati wa harakati za kudai uhuru.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, amesisitiza kuwa kuimarika kwa utalii katika Ziwa Nyasa kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ameweka wazi kuwa sekta hiyo itatengeneza ajira kupitia huduma za malazi, usafiri, na uvuvi wa kitalii, huku ikihimiza utunzaji wa mazingira na urithi wa kitamaduni kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464