` VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA MAOMBI KWA TAIFA, RAIS NI AGIZO LA MUNGU

VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA MAOMBI KWA TAIFA, RAIS NI AGIZO LA MUNGU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito mzito kwa viongozi wa dini nchini, akiwataka kutekeleza wajibu wao wa kiroho kwa kuliombea Taifa na kumuombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Wito huu wa kuliombea Taifa na viongozi wake japo umekumbuishwa na Dk Nchimbi kiukweli si jambo la hiari, bali ni agizo kuu la kiroho linalolenga kuhakikisha nchi inabaki katika utulivu na heri.

Dk. Nchimbi akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusimikwa kwa Uongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPTC).

Katika Biblia  katika kitabu cha 1 Timotheo 2:1-2, inasisistizwa kufanyika kwa dua na sala kwa ajili ya wenye mamlaka ili watu waishi kwa amani.Pia mafundisho ya Kiislamu katika Kurani (4:59), inahimizwa utii na kumuombea kiongozi ili apate 'Tawfiq' au muongozo wa Kimungu katika kuwatumikia watu kwa uadilifu.

Tunapomuombea Rais wetu, tunaliombea Taifa letu afya. Biblia inasema katika Mithali 29:2 kuwa 'wenye haki wakiwa na mamlaka, watu hufurahi', hivyo maombi  ndiyo yanayofanya wananchi waendelee kufurahia amani na maendeleo .

Mbali na hayo, Makamu wa Rais alikemea mmomonyoko wa maadili na rushwa, akirejea misingi ya imani kuwa mwanadamu anapaswa kuwa mwaminifu. Aliwataka viongozi wa dini kusimamia malezi ya vijana ili kujenga taifa linalomcha Mungu na kuheshimu utu, akisisitiza kuwa "taifa bila maadili ni taifa lililopotea."

Pia, aligusia suala la uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya ibada. Alisema kuwa kulinda uumbaji wa Mungu ni jukumu la kila muumini, hivyo akahimiza viongozi wa dini kutumia mimbari zao kukemea ukataji miti na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa vizazi vijavyo.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa dua maalum kuliombea Taifa, huku Dk. Nchimbi akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu na kuhakikisha kuwa amani ya Tanzania inabaki kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote.

Aidha katika kuonyesha kwa vitendo ushirikiano wa Serikali na dini, Dk. Nchimbi alitangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa eneo la ekari 12 mkoani Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya CPTC, sambamba na mchango wa Sh. milioni 100 kuanzisha ujenzi huo. Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha taasisi za dini ambazo zimekuwa washirika wakubwa wa serikali katika elimu na afya.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464