.jpg)
KATIKA wimbi jipya la kuamsha uzalendo miongoni mwa vijana nchini, wadau mbalimbali wametoa tahadhari kwa vijana kuepuka watu wanaochochea uharibifu na kusambaza maneno ya uongo yenye lengo la kupindisha ukweli kuhusu hali ya nchi.
Wito huo umekuja wakati Tanzania ikijipanga kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, ambapo utulivu wa kisiasa na kijamii unatajwa kama nguzo mama itakayowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uwezeshaji wa vijana kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya vijana na wanadiplomasia, Mratibu wa Makongamano nchini, Omary Punzi, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli kwa kuzingatia mafundisho ya viongozi wa dini ambayo yanahimiza upendo na mshikamano.
“Watanzania tunapaswa kuwa wazalendo wa nchi yetu, hii ni tunu ya taifa. Jamii inapaswa kusimamia amani ya nchi na maadili ambayo yatatufanya tuwe na uvumilivu wa kukabili changamoto. Mshikamano ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi,” alisema Punzi.
Aliongeza kuwa katika ulimwengu wa sasa wa mitandao ya kijamii, kuna kundi la watu limekuwa likitumia lugha za upotoshaji na kupindisha ukweli ili kuleta taharuki, jambo alilosema vijana wanapaswa kuwa macho nalo ili wasitumiwe kama daraja la kuvuruga amani.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Simbani, Kibaha, Pili Machibya, amewasihi wananchi, hususan vijana, kutunza amani waliyoikuta tangu kuzaliwa. Alibainisha kuwa mshikamano na kuvumiliana ndiyo siri ya mafanikio ya Tanzania tangu enzi za waasisi wa taifa.
“Tutunze amani yetu kwa kushikamana na kuachana na mifarakano kwani tangu tunazaliwa tumeikuta amani na tumezoea kuvumiliana. Ni jambo jema na la busara kwani bila uvumilivu mambo hayawezi kwenda vizuri,” alisisitiza Machibya.
Naye mkazi wa Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani, Walles George, alionya kuwa gharama ya kupoteza amani ni kubwa kiasi kwamba hakuna mwananchi anayeweza kuimudu. Alisema kuwa utulivu wa nchi ndiyo unaomfanya kijana aweze kutoka asubuhi kwenda kutafuta riziki bila hofu.
“Tusikubali kuipoteza amani yetu kwani ikipotea gharama yake ni kubwa sana. Hii ni tunu ambayo tumetunukiwa, hivyo lazima tuilinde na tuwaepuke wale wanaotaka kuiharibu. Utulivu ni jambo muhimu kwani unatufanya tuweze kutoka na kufanya shughuli zetu,” alisema George.
Ujumbe wa wadau hawa unaenda sambamba na msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imekuwa ikihimiza falsafa ya 4R (Reconciliation, Resiliency, Reforms, and Rebuilding). Wadau hao wamebainisha kuwa bila uvumilivu (Resiliency), taifa haliwezi kufanya mageuzi ya kweli ya kiuchumi yanayohitajika kuelekea mwaka 2050.
Hivyo, vijana wamehimizwa kuwa mstari wa mbele kusema ukweli, kupiga vita taarifa za kizushi (fake news), na kuelekeza nguvu zao katika fursa za uwezeshaji zinazotolewa na serikali na sekta binafsi badala ya kujiingiza katika migogoro isiyo na tija kwa taifa.