
Sekta ya utalii nchini Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa na wa kihistoria, ikichochewa na jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Sita.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa idadi ya watalii wa nje imeongezeka kutoka 2,141,895 mwaka 2024 hadi kufikia 2,294,495 mwaka 2025. Hali kadhalika, utamaduni wa utalii wa ndani umeimarika, ambapo idadi ya watalii wazalendo imepanda kutoka milioni 3.2 hadi milioni 3.6 katika kipindi hicho.
Mafanikio haya yamepelekea kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni, ambapo sekta hiyo imeingiza Dola za Marekani milioni 3.9 mwaka 2024 ikilinganishwa na milioni 1.3 mwaka 2021. Juhudi hizi zimepata msukumo mkubwa kupitia filamu za kimkakati za "Tanzania: The Royal Tour" na "Amazing Tanzania". Filamu hizi zimeongeza utambulisho wa nchi duniani na kuvutia wimbi jipya la wawekezaji na watalii.
Takwimu hizo zimetolewa na Msemaji Mkuu wa serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es salaam Februari 26, mwaka huu.
Alisema kutokana na uboreshaji wa vivutio, Tanzania imeshinda tuzo mbalimbali za kimataifa kupitia World Travel Awards (WTA) mwaka 2024 na 2025. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kutambulika kama Hifadhi Bora ya Taifa Duniani kwa miaka sita mfululizo kuanzia 2019 hadi 2024. Mlima Kilimanjaro nao umetawala kama kivutio bora cha utalii barani Afrika.
Aidha, Tanzania imetangazwa kuwa kivutio bora zaidi cha safari za nyikani (Safari Destination) duniani kwa mwaka 2024 na 2025. Mafanikio haya yameimarisha imani ya watalii wa kimataifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii barani Afrika. Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya anga, reli, na barabara ili kurahisisha ufikiaji wa vivutio hivi.
Ukuaji huu si tu unaongeza mapato, bali pia unachochea sekta nyingine kama hoteli, usafirishaji, na biashara ndogo ndogo. Serikali inalenga kuendeleza kasi hii ili sekta ya utalii iendelee kuwa mhimili mkuu wa uchumi wa taifa. Kwa ujumla, sekta hii sasa inachangia kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464