Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekutana na Mkurugenzi mtendaji Benki ya Azania Bi. Esther Mangenya na kufanya mazungumzo ya namna bora ya kushirikiana katika kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi, elimu msingi na ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja miundombinu ya huduma nyinginezo za kijamii.
Prof. Shemdoe alifanya mazungumzo hayo na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya Azania tarehe 05 Februari 2026 ofisini kwake Jijini Dodoma, alipomtembelea kwa lengo la kujitambulisha ili kujenga mahusiano mazuri ya kiutendaji yatakayowanufaisha wananchi waliopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Katika kikao kazi hicho, Prof. Shemdoe na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania Bi. Esther Mangenya wamekubaliana kujenga mahusiano mazuri ili wananchi wanufaike na mchango wa Serikali na benki hiyo katika kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za kijamii.
Kwa kutambua mchango wa taasisi za kifedha kwa jamii, Prof. Shemdoe amesema ofisi yake ipo tayari kushirikiana na benki hiyo na kuitambulisha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili waifikie jamii na kuihudumia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania Bi. Esther Mangenya amemueleza Prof. Shemdoe kuwa benki yake imedhamiria kuwajibika kwa jamii kwa kutoa mchango utakaoboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwepo na za kifedha.
Prof. Shemdoe tangu apewe dhamana na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa, amekuwa mstari wa mbele katika kukutana na Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuboresha ushirikiano na ofisi ili kupeleka tabasamu kwa wananchi na ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464





