Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini Rehema Nhamanilo,akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga(Shinyanga Girls) baada ya kutembelea shule hiyo. 
Nhamanilo ametoa wito huo leo wakati wa ziara yake shuleni hapo iliyopo Mtaa wa Butengwa, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika ziara hiyo ameambatana na Kamati ya utekelezaji ya UWT Wilaya pamoja na makatibu na wenyeviti wa UWT Kata zote za Shinyanga Mjini.
Akizungumza na wanafunzi, Nhamanilo amesema UWT imefika shuleni hapo kama wazazi wa karibu kwa lengo la kuwapa mawaidha na kuwatia moyo wasichana hao.
“Tumekuja kuzungumza nanyi kama wazazi wenu. Tunawasihi msome kwa bidii, msikubali kudanganywa kwa chips au kushawishiwa na wanaume ambao hawawatakii mema. Kataeni na semeni tunasonga mbele,” amesema Nhamanilo.
Aidha, amewahimiza wanafunzi kupendana, kuheshimiana na kusameheana wanapokoseana pamoja na kusaidiana katika masomo. Ameongeza kuwa UWT ipo tayari kutoa ushauri pale wanapohitaji msaada.
“Mnapohitaji ushauri muoneni matroni wenu, lakini pia sisi tupo karibu ofisini na tuko tayari kuwasaidia,” ameongeza.
Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Shinyanga Girls, Simon Lange, ameishukuru UWT Wilaya ya Shinyanga kwa zawadi walizokabidhi ambazo ni taulo za kike, akisema zitasaidia wanafunzi wenye uhitaji kujisitiri wakati wa hedhi.
Lange ameeleza kuwa shule hiyo ilianzishwa tarehe 13 Agosti 2023 ikiwa na wanafunzi 73, na hadi kufikia mwaka 2026 imefikia wanafunzi 859. Ameongeza kuwa shule hiyo mafanikio makubwa kielimu katika Manispaa ya Shinyanga.

“Kwa matokeo ya Kidato cha Pili mwaka 2025, shule imeongoza Manispaa ya Shinyanga ambapo wanafunzi 107 walipata Daraja la Kwanza, 12 Daraja la Pili na 3 Daraja la Tatu,” amesema Lange.
Kwa niaba ya wanafunzi, Astelia Kimese, ameishukuru UWT Wilaya ya Shinyanga kwa kuwakumbuka na kuwapatia taulo za kike, akisema zitawasaidia wasichana wenye uhitaji kuendelea na masomo bila changamoto wakati wa hedhi.

Kwa upande wake Kaimu Katibu wa UWT Wilaya ya Shinyanga Naibu Katalambula , ambaye pia ni Katibu wa UVCCM Wilaya, amesema UWT imeamua kuwatembelea wanafunzi hao ili kuwapa moyo na kuwafanya wajisikie kuwa na wazazi wanaowajali.
“Tumekuja kuwasalimia, kuwatia moyo na kuhakikisha mnajisikia furaha. Tumeleta zawadi kidogo kama ishara ya upendo wetu. Tunawasihi mzingatie masomo ili baadaye muwe viongozi, kwani lengo la shule hii ni kuwaandaa wasichana kielimu na kuwajengea kujiamini katika uongozi,” amesema Katalambula.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464








