` MIZENGO PINDA: MAHUSIANO NI MSINGI WA AMANI, UMOJA NA MAENDELEO YA TAIFA

MIZENGO PINDA: MAHUSIANO NI MSINGI WA AMANI, UMOJA NA MAENDELEO YA TAIFA

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, amesema mahusiano ni mchakato unaojengwa kwa misingi ya mazungumzo na uelewano, akisisitiza umuhimu wa kuwa na lugha moja ndani ya jamii ili kudumisha amani na umoja wa Taifa.
Mheshimiwa Pinda alitoa kauli hiyo alipokutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, Februari 12, 2026 nyumbani kwake mstaafu huyo jijini Dodoma.
Pamoja na kumpongeza Mhe. Sangu kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kusimamia Sekta ya Mahusiano na kumtaka kuendeleza mahusiano bora na wananchi pamoja na wadau wote wanaomzunguka, alisema mahusiano ni msingi muhimu katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa.

Waziri Sangu, alimtembelea Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, nyumbani kwake Jijini Dodoma kupata uzoefu na ushauri kuhusu ujenzi na uimarishaji wa mahusiano katika jamii, kufuatia kuanzishwa kwa Kitengo cha Mahusiano na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kitengo hicho kinatakiwa kujenga na kuimarisha mshikamano na kuwa na mwelekeo mmoja katika sekta za kidini, kiraia na nyinginezo kwa ajili ya ustawi wa Mama Tanzania.

Mhe. Sangu alimwambia Waziri Mkuu mstaafu kuwa tayari wameanza kukutana na viongozi wa dini mbalimbali wakiwemo The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT), Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Kanisa la Waadventista wa Sabato.

Mhe. Sangu amempongeza Mhe. Pinda kwa mchango wake katika kuasisiwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Amani ya Viongozi wa Dini, akieleza kuwa uzoefu wake katika masuala ya migogoro ya kijamii ni hazina muhimu katika kuimarisha sekta ya mahusiano nchini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464