` MSHIKAMANO NA AMANI: NGAO YETU DHIDI YA WANAOTAKA KUTUFARAKANISHA

MSHIKAMANO NA AMANI: NGAO YETU DHIDI YA WANAOTAKA KUTUFARAKANISHA

Katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea maendeleo makubwa, sauti za wadau mbalimbali nchini zimeungana kusisitiza jambo moja kuu: kulinda amani ya nchi kwa wivu mkubwa huku tukiwapuuza na kuwadharau wale wote wanaojaribu kupanda mbegu za chuki na mafarakano miongoni mwa Watanzania. 

Amani imetajwa kuwa si tu tunu ya kitaifa, bali ni msingi wa maisha na ustawi wa kila mwananchi, kuanzia mfanyabiashara mdogo hadi viongozi wa juu.

Katibu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mkoa wa Pwani, Godfrey Lucas, anatoa onyo kali dhidi ya tabia za baadhi ya watu wanaotaka kuigawa nchi kwa misingi ya udini, ukabila, na rangi. 

Anasisitiza kuwa suala la kulinda utulivu wa nchi si jukumu la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila raia. Kwa mujibu wa Lucas, gharama ya kurejesha amani ni kubwa mno kulinganisha na gharama ya kuitunza, hivyo ni lazima Watanzania wawe na mshikamano wa dhati na kuwapuuza wale wenye tabia mbaya za kutaka kuivuruga nchi kwa maslahi yao binafsi.

Dhana hii ya mshikamano inaungwa mkono na wadau wa maendeleo mkoani Pwani, akiwemo Mwenyekiti wa Wajasiriamali Maili Moja A, Abdul Juma, ambaye anaelezea amani kama kitovu cha maendeleo ya kiuchumi. Kwake yeye, bila utulivu hakuna mwananchi anayeweza kutoka nje kutafuta riziki yake. 

Hivyo, tunapaswa kuitazama amani kama ngao inayotuwezesha kufanya shughuli zetu kwa uhuru na mshikamano. Huu ni ujumbe wa wazi kwa wanaojaribu kutufarakanisha: kuwa Watanzania ni wamoja na hawapo tayari kuchezewa amani yao.

Aidha, sauti kutoka kwa viongozi wa kiroho na kijamii zinaendelea kupigilia msumari umuhimu wa kuaminiana. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, anasisitiza kuwa jadi ya nchi yetu ni utulivu na hakuna nafasi kwa ubaguzi. 

Vilevile, Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF), Rosemary Bujashi, anahimiza kuwa amani ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote, huku akiwataka Watanzania kujiweka mbali na wale wasioitakia mema nchi yetu na wanaolenga kutugawa.

Kwa upande wa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa, mwito umetolewa wa wao kujiepusha na makundi yanayoweza kuyumbisha nchi kiuchumi na kijamii. 

Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, amewasihi vijana kuacha makundi yanayorudisha nyuma juhudi za maendeleo na badala yake wahubiri upendo. 

Anasema kuwa utulivu unavutia wawekezaji na kuwapa viongozi nafasi ya kutekeleza majukumu yao bila hofu. Kwa ujumla, ujumbe ni mmoja: Watanzania tuwe na wivu na nchi yao, tuwapuuze wafitini, na tusimame imara kulinda amani yetu ambayo ndiyo utambulisho wetu mkuu barani Afrika. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464