
SERIKALI ya Awamu ya Sita imefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa vijana wabunifu na wataalamu wa teknolojia nchini, kufuatia tangazo la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu kukamilika kwa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Programu za Anga za Juu (2025–2030).
Mpango huo, ambao unatekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unalenga kuifanya Tanzania kuwa na satelaiti yake na kuimarisha ushiriki wa nchi katika uchumi wa anga za juu kimataifa.
Mpango huo umejikita katika nguzo kuu tano ambazo ni kuweka mfumo wa utawala na sera, kuimarisha uwepo wa Tanzania kimataifa, kuendeleza rasilimaliwatu na tafiti, kujenga miundombinu ya anga, na kukuza matumizi ya teknolojia hiyo katika sekta zote.
Kwa vijana wabunifu, hii ni fursa ya dhahabu kwani serikali imepanga kuanza utungaji wa Sera na Sheria ya Anga za Juu ya Mwaka 2026, hatua itakayoweka mazingira rafiki kwa wabunifu wa ndani kushiriki katika miradi mikubwa ya kisayansi.
Uchambuzi wa mpango huo unaonyesha kuwa, matumizi ya teknolojia ya satelaiti yataenda kugusa moja kwa moja sekta za kilimo, madini, mazingira, na uchumi wa bluu (baharini).
Hii ina maana kuwa "Machampioni wa Sayansi" nchini sasa wana uwanja mpana wa kutengeneza mifumo na programu tumizi (Apps) zinazoweza kutumia data za anga kutatua changamoto za kijamii, jambo ambalo litaongeza thamani ya ubunifu wao na kutengeneza ajira za kisasa zinazokwenda na kasi ya ulimwengu wa kwanza.
Aidha, wizara imesisitiza kuwa mwelekeo huu mpya utasaidia nchi kuwa na sauti ya pamoja katika tafiti na matumizi ya teknolojia ya anga.
Kwa vijana wa kike na kiume waliojikita katika masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu), hatua hii ni kielelezo kuwa serikali imesikia kilio chao cha kutaka mazingira wezeshi ya kitafiti.
Ni wazi kuwa kupitia mpango huu, Tanzania haitakuwa mtumiaji tu wa teknolojia za nje, bali mzalishaji na mshindani katika soko la kimataifa la teknolojia ya anga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464