` MBUNGE AZZA HILAL AOMBA BARABARA YA DIDIA–SOLWA IPANDISHWE HADHI 'IWEKWE LAMI'

MBUNGE AZZA HILAL AOMBA BARABARA YA DIDIA–SOLWA IPANDISHWE HADHI 'IWEKWE LAMI'

 


Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akiwa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hilal Hamad, ameomba Serikali kuipandisha hadhi barabara ya Didia–Solwa ili iweze kuhudumiwa kwa kiwango kinachostahili kulingana na umuhimu wake kiuchumi na kijamii.

Maombi hayo ameyatoa Februari 24, 2026 katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa.

Mhe. Azza amesema uboreshaji wa barabara hiyo utarahisisha usafirishaji wa mazao, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa Didia na Solwa. Sambamba na hilo, ameomba kuwekewa lami kipande cha barabara kutoka njiapanda ya Didia (Puni) hadi Didia Senta ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya biashara katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa Didia Senta inatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha uchumi kutokana na ujenzi wa Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR), hivyo uboreshaji wa barabara hiyo utawezesha mtiririko mzuri wa watu na mizigo na kunufaisha wananchi pamoja na wawekezaji.

Aidha, amesisitiza kuwa barabara ya Didia–Solwa ikipandishwa hadhi, itaanza kusimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) badala ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua ambayo itaipa uzito wa kitaifa na kuongeza uwezo wa kupata rasilimali za kutosha kwa ajili ya matengenezo na maboresho ya kudumu.

Halikadhalika, Mhe. Azza ameomba pia barabara ya Didia/Kabanga/Mwamalulu kwenda Isakajana katika Jimbo la Msalala ipandishwe hadhi, hatua itakayorahisisha usafiri wa wananchi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya mikoa na wilaya zinazozunguka eneo hilo.

Katika kuimarisha usalama barabarani, Mbunge huyo pia ameiomba Serikali kuweka taa za barabarani katika njiapanda ya Tinde na Didia pamoja na kufunga taa za kuongozea magari katika njiapanda ya Tinde, kufuatia ongezeko la magari na watembea kwa miguu katika maeneo hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kupitia TANROADS na TARURA, huku akisisitiza usimamizi madhubuti ili kulinda uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta hiyo.

“Suala la taa ni kipaumbele. Waheshimiwa wabunge wamezungumzia uwepo wa taa katika maeneo mbalimbali, hatua ambayo imechochea ukuaji wa maeneo na mzunguko wa kiuchumi. Tunaangalia namna ya kuongeza taa, mfano pale Tinde, ambayo ni moja ya senta zinazohitaji taa za uhakika,” amesema Mhita.

“Ajenda ya Barabara ya Kolandoto ni kipaumbele cha mkoa wa Shinyanga. Kuhusu barabara ya Didia–Solwa, Mhe. Mbunge Azza Hilal ameomba ipandishwe hadhi. Kwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga yupo hapa, anajua hatua za haraka kuchukua ndani ya wiki hii. Andiko la barua litufikie mkoani ili tuweze kusukuma barabara yetu ipandishwe hadhi kutoka TARURA hadi TANROADS, na hatimaye kuipatia fedha za lami”,ameongeza Mhe. Mhita.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464