` GCI YATOA MSAADA WA TAULO ZA KIKE SHULE YA SEKONDARI IMENYA, SHINYANGA

GCI YATOA MSAADA WA TAULO ZA KIKE SHULE YA SEKONDARI IMENYA, SHINYANGA

 



Na Mwandishi wetu.

Shirika lisilo la kiserikali la Green Community Initiative (GCI) la Manispaa ya Shinyanga, linalojihusisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga, limetoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya sekondari Imenya.

Msaada huo umetolewa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya taaluma kwa watoto wa kike, ili waweze kushiriki masomo kwa muda wote bila kukumbwa na changamoto ya utoro wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afisa Fedha wa shirika la  GCI,Maryciana William Vahaye ,anasema kuwa baadhi ya wasichana mkoani Shinyanga wamekuwa wakikosa masomo wakati wa hedhi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mwamko mdogo wa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa ununuzi wa pedi, mila na desturi za kijamii, pamoja na hali duni ya uchumi katika familia nyingi.

“Msaada huu unalenga kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki yao ya elimu bila vikwazo vinavyotokana na mabadiliko ya miili yao. Tunahitaji kuona wanafunzi wa kike wanakuwa na ufaulu mzuri kitaaluma katika shule hii na maeneo mengine,” amesema Maryciana

Aidha, GCI pia ilitoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu matumizi sahihi ya taulo za kike, ikiwemo namna ya kuzifua na kuzianika katika joto la jua kwa usahihi ili kuepuka madhara ya fangasi au maambukizi mengine.

Mmoja wa wanafunzi, Rose Kashinje, aliishukuru GCI kwa msaada huo akisema utawasaidia kuongeza mahudhurio shuleni na kuboresha ufaulu wao.

Nashukuru shirika la GCI kwa kutuletea taulo za kike. Hii itatusaidia kuongeza mahudhurio na kufanya vizuri zaidi katika masomo yetu,” alisema Rose.

Wanafunzi hao pia waliwataka wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za upatikanaji wa taulo za kike shuleni ili kusaidia ukuaji wa kitaaluma kwa watoto wa kike na kupunguza utoro unaotokana na changamoto za hedhi.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464