SERIKALI YAPUNGUZA ADA ZA LESENI KWA WATOA MAUDHUI MTANDAONI
Na Marco Maduhu, DODOMA
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepunguza ada za leseni kwa watoa huduma na wakusanya maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikikabili sekta hiyo na kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidigitali.
Akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vya utangazaji 2026 unaofanyika Dodoma kwa siku mbili, kuanzia leo Februari 12 hadi kesho, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Serikali iliiagiza TCRA kufanya mapitio ya ada hizo baada ya malalamiko ya wadau kuhusu gharama kuwa kubwa.
Amesema mapitio hayo yamekamilika na kuleta nafuu kubwa kwa watoa maudhui, hususan vijana wabunifu na wajasiriamali wanaotumia majukwaa ya mtandaoni.
“Nafuraha kuwafahamisha kwamba mapitio hayo yamefanyiwa kazi na kuleta historia kwa watoa maudhui mtandaoni, ada za leseni zimepunguzwa kwa kiwango kikubwa kutoka Sh 500,000 hadi Sh 50,000, na ada ya maombi itakuwa Sh 10,000 tu, kwa upande wa wakusanya maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepungua kutoka Sh milioni moja hadi Sh 100,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh 20,000 tu,” amesema Mwinjuma.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha urasimishaji wa shughuli za kidigitali, kupanua fursa kwa vijana wabunifu, kuchochea ajira na kuongeza mchango wa uchumi wa kidigitali katika pato la taifa.
Katika hatua nyingine, Mwinjuma amesema mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa waandishi wa habari, hayawezi kuzaa matunda iwapo maslahi yao hayatapewa kipaumbele.
Amesema, baadhi ya waandishi hawana mikataba rasmi, na hulipwa stahiki zao kwa kuchelewa, hali inayodhoofisha sekta hiyo.
“Naiagiza TCRA kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unaenda sambamba na uthibitisho wa mikataba na malipo stahiki kwa wafanyakazi,” amesema Mwinjuma.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kushughulikia suala la madeni ya matangazo ya Serikali yanayodaiwa na vyombo mbalimbali vya habari, kwa lengo la kuhakikisha yanalipwa kwa wakati na kusaidia mzunguko wa fedha katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, amesema mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa sekta ya utangazaji kujadili changamoto na fursa zilizopo.
Amesema hadi kufikia Desemba 2025, TCRA ilikuwa imetoa leseni 707, zikiwamo leseni 258 za redio, 73 za televisheni, 318 za vyombo vya mtandaoni, 55 za huduma za waya, na leseni tatu za huduma za usikivu mtandaoni.
Baadhi ya watoa maudhui mtandaoni, wameipongeza Serikali kwa uamuzi huo, wakisema utawasaidia wengi kurasimisha shughuli zao na kufanya kazi kwa uhuru na weledi zaidi katika kuhabarisha umma.
kaulimbiu ya mkutano mkuu wa mwaka huu ya vyombo vya utangazaji inasema “Matumizi ya Teknolojia katika kupanua na kuboresha huduma za utangazaji vijijini,” ikilenga kuhakikisha huduma za utangazaji zinafika maeneo ya vijijini na kuibua fursa za kiuchumi.
TAZAMA PICHA👇👇
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, akizungumza.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, akizungumza.
Mkutano ukiendelea.























