` WAANDISHI WATAKIWA KUANDIKA HABARI KWA WELEDI MASUALA YA EWURA

WAANDISHI WATAKIWA KUANDIKA HABARI KWA WELEDI MASUALA YA EWURA


Na Marco Maduhu, Dar es Salaam

Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia misingi ya taaluma kwa kuandika habari kwa usahihi, weledi na kwa kuzingatia uwiano wanaporipoti masuala ya sekta ya nishati na maji, ili kuiwezesha jamii kupata taarifa sahihi na zenye manufaa.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA Tanzania).
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Lorivii Long’idu, amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuhabarisha umma kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, hivyo vinapaswa kuandika taarifa kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Amesema, warsha hiyo ni muhimu kwa waandishi wa habari na ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya EWURA, kwani kadri wanavyopata uelewa sahihi ndivyo umma unavyonufaika kupitia taarifa wanazoziandika.
“Tunapowapa waandishi uelewa sahihi kuhusu EWURA, tunaiwezesha jamii kupata taarifa zilizo sahihi na zenye manufaa,” amesema Long’idu.

Naye Mwenyekiti wa MISA Tanzania Edwini Soko, amesema mafunzo hayo ni mrejesho wa warsha iliyofanyika Juni 16 mwaka jana, ambapo waandishi wa habari waliandika jumla ya habari 103 zilizohusu shughuli na majukumu ya EWURA.
Amesema, warsha ya sasa ni muendelezo wa ushirikiano kati ya MISA Tanzania na EWURA katika kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari ili kuifahamu vyema mamlaka hiyo na kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa taarifa sahihi.

“Muendelezo wa warsha hizi ni kuendelea kutengeneza waandishi ‘champions’ wa kuandika habari kwa usahihi na weledi zinazohusu majukumu ya EWURA,” amesema Soko.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, waandishi wataendelea kuandika habari zinazohusu EWURA kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi wa habari na kuimarisha uwajibikaji kwa jamii.

TAZAMA PICHA👇👇
Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Lorivii Long’idu, akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa EWURA.
Mwenyekiti wa Misa-Tanzania Edwin Soko akizungumza.
Mwenyekiti wa Misa-Tanzania Edwin Soko akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464