Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, amefanya mkutano mkubwa wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Samia Suluhu Hassan, na kumchagua tena yeye kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mkutano huo umefanyika leo Februari 22, 2026 katika Viwanja vya Zimamoto, Shinyanga, ukihudhuriwa na mamia ya wananchi, wanachama wa CCM pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.
Akizungumza katika mkutano huo, Katambi amesema amekuja kutoa shukrani kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kumuamini kwa mara nyingine tena, na kuwaahidi kuendeleza kasi ya maendeleo aliyoanza nayo katika awamu iliyopita.
“Nawashukuru sana wananchi wa Shinyanga kwa kuniamini na kunichagua tena niwe mbunge wenu, pamoja na kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025. nawahakikishia kasi ya maendeleo inaendelea,” amesema Katambi.
Pia amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumwamini na kumteua tena kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akiahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu na kwa maslahi ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Katambi amemuonya mkandarasi anayejenga stendi ya mabasi ya kisasa na barabara ya lami kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, akimtaka kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo au aachie kazi kabla hajachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maendeleo jimboni humo, kuhakikisha wanazingatia mikataba yao, kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
"Ukicheka na nyani, utavuna mabua, haiwezekani Rais anatoa pesa za miradi ya maendeleo, lakini Wakandarasi wachache wanataka kuzichezea, kwa cheo changu nilichonacho cha Waziri wa Mambo ya ndani, mtaipata fresh," ameongeza Katambi.
Amewaonya pia watumishi wazembe na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa au kuwaonea wananchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi, akisisitiza kuwa serikali inasimamia haki na usawa kwa wote.
Amewataka pia wananchi wa Shinyanga na taifa kwa ujumla kuendelea kudumisha amani kwa kufuata Katiba, sheria na miongozo ya nchi ili kulinda utulivu uliopo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amempongeza Katambi kwa kuendelea kuaminiwa na Rais, na kumtaka kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho, vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kusogeza huduma katika ngazi ya kata.
Amesema wananchi wengi hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo wilayani, hali inayowaongezea gharama.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamempongeza Katambi kwa kuitisha mkutano wa shukrani, na kuomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
TAZAMA PICHA 👇👇
Katambi akizungumza na wananchi wa Shinyanga.
Katambi akiwashukuru wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa (kulia) akiwa na Mbunge Katambi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anorld Makombe akizungumza.
Mbunge wa Vitimaalumu Mkoa wa Shinyanga Mwanahamisi Munkunda na Mjumbe wa SADC akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Katambi akiteta jambo na Mwenyekiti wa CCM Mabala Mlolwa.