` SERIKALI YAONDOA MASHARTI MAGUMU MIKOPO YA VIJANA

SERIKALI YAONDOA MASHARTI MAGUMU MIKOPO YA VIJANA



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Serikali imeondoa masharti magumu yaliyokuwa kikwazo kwa vijana kunufaika na mikopo, likiwamo sharti la dhamana isiyohamishika, ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fedha za uwezeshaji Sh bilioni 200 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.
Hayo yamebainishwa leo Februari 21, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati akizungumza na vijana wa Mkoa wa Shinyanga katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Vijana mkoani humo.

Nanauka amesema masharti yaliyokuwa yanawakwamisha vijana wengi kupata mikopo sasa yamefutwa, ikiwamo dhamana isiyohamishika, huku marejesho yakianza kati ya miezi mitatu hadi sita baada ya kupokea mkopo, ili kuwapa muda wa kukuza miradi yao.

“Ninafuraha kuwaambia kwamba fedha ambazo Rais Samia aliahidi kutoa kwa ajili ya vijana, Sh bilioni 200, tayari nimeshazipokea na Waziri Mkuu ndiye alinikabidhi hundi ya fedha hizi, na baadhi ya vijana wameanza kunufaika nazo,” amesema Nanauka.
Amesema fedha hizo zimetengwa mahsusi kwa ajili ya vijana na zimesambazwa katika sekta mbalimbali zikiwamo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu.

Ameeleza kuwa dhamira ya Rais ni kuona vijana wanakuwa wabunifu, wachapakazi na kuinuka kiuchumi, akitoa mfano wa vijana wa Mkoa wa Mwanza ambao tayari wamepatiwa Sh. milioni 200 kupitia mpango huo.
Aidha, amesema Serikali itaanzisha dawati maalumu la vijana ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) litakaloshughulikia masuala ya kodi kwa vijana ili kuwawekea mazingira rafiki ya ulipaji na uendeshaji wa biashara.

Katika hatua nyingine, amewataka vijana kuwa na ndoto, nidhamu ya muda na kujituma katika kufikia malengo yao, akisisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa inayochangia asilimia 55 ya uzalishaji nchini.

“Serikali imeamua kuwekeza kwa vijana na kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha, pamoja na kuwajengea ujuzi kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), na tayari imetoa Sh bilioni 3 na vijana wengi wapo VETA,” amesema Nanauka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo, ikiwamo kuanzisha viwanda vidogo, akisema maeneo ya uwekezaji yametengwa na fedha zipo za kuwawezesha.

Baadhi ya vijana walioshiriki uzinduzi wa jukwaa hilo wamesema kuondolewa kwa masharti magumu ni faraja kubwa na kutawawezesha wengi kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na Serikali.

TAZAMA PICHA👇👇
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akizungumza na vijana mkoani Shinyanga wakati akizundua Jukwaa la Vijana mkoani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka akizungumza na vijana mkoani Shinyanga wakati akizundua Jukwaa la Vijana mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Vijana mkoani humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464