Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amewataka watumishi wa Afya wilayani humo, kutoa huduma bora kwa wananchi, huku akiagiza Daktari wa Hospitali ya wilaya hiyo Stephano Badiana, na Muuguzi Msafiri Kulwa, wahamishwe kwa muda hospitalini hapo na kupangiwa vituo vingine vya kazi, kufuatia tuhuma za kutoa huduma mbovu na kuomba rushwa wagonjwa.
Amefanya kikao hicho jana katika ukumbi wa Hospitali ya wilaya ya Shinyanga.
Amesema, Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa ikitoa fedha za kuboresha huduma za afya, na hivyo kuwataka watumishi wa afya wilayani humo, wajikite kutoa huduma bora za afya kwa kuendena na kasi ya Rais Dk. Samia, na kwamba watumishi wazembe na wanaotaka kukwamisha ubora wa huduma watawajibishwa.
Amesema katika hospitali hiyo ya wilaya ya Shinyanga, amekuwa akipokea malalamiko ya Daktari Stephano Badiana kwa utoaji huduma mbovu , kuendekeza vitendo vya Rushwa , kuchukua hela nje ya mfumo, pamoja na Muuguzi Msafiri Kulwa ambaye naye amekuwa na mwenendo mbovu wa kuhudumia wagonjwa.
“Mganga Mkuu, Daktari huyu na Muuguzi wake, naagiza wahamishiwe kwenye vituo vingine vya kazi kwa muda na siyo hapa, sijasema wasimamishwe kazi, bali watafutiwe vituo vingine vya kazi kwa muda hadi pale timu zangu zimalize uchunguzi,” amesema Mtatiro.
“Takukuru ingieni kazini, shughulikieni malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na mwenendo wake, na kugueni hadi mifumo ambayo amekuwa wakiifanyia kazi daktari huyu,” ameongeza Mtatiro.
Aidha, amewaonya pia watumishi wengine ambao ni Emmanuel Zakayo na Majiji Mayunga kwa mienendo yao mibaya ya utoaji huduma, pamoja na kuwarubuni wagonjwa kwa kuanzisha ajenda zingine kwa kutengeneza mpango wa kando ndipo wapate kuwatibu, na kwamba atakaa nao kikao cha wababa ili kuwarekebisha.
Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa afya wilayani humo, kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, kutumia mfumo wa Butomizi ili kudhibiti mapato ya hospitali, pamoja na kutoa dawa kwa wangonjwa, na siyo kuwambia wanakununue kwenye maduka binafsi na wakati dawa zipo hospitalini za kutosha.
Amesisitiza kuwa, serikali haitavumilia vitendo vya rushwa na uzembe kazini, hasa katika sekta ya afya inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, na kwamba mtumishi atakayekwenda kinyume na maadili ya utumishi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Na baadhi ya watumishi hao, wamesema kikao hicho kimewakumbusha wajibu wao na kwamba watazingatia maelekezo yote ya Mkuu huyo wa wilaya.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza na watumishi Sekta ya Afya wilayani Shinyanga.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akizungumza.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk. Nuru Yunge akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464