` MBUNGE AZZA ATOA MKONO WAPONGEZI SHULE YA MSINGI MASUNULA KUFAULISHA WANAFUNZI WOTE 30 KWA DARAJA “A”

MBUNGE AZZA ATOA MKONO WAPONGEZI SHULE YA MSINGI MASUNULA KUFAULISHA WANAFUNZI WOTE 30 KWA DARAJA “A”

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amefanya hafla fupi ya kuwapongeza walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Masunula iliyopo Kata ya Usule wilayani Shinyanga, baada ya wanafunzi wote 30 kufaulu Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba (2025) kwa daraja “A”.

Kutokana na ufaulu huo, wanafunzi 18 wamechaguliwa kujiunga na shule maalumu za bweni, huku wanafunzi 12 wakipangiwa kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Igalamya wilayani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Azza amesema ametoa mkono wa pongezi kwa shule hiyo kama motisha kwa shule nyingine za msingi ndani ya Jimbo la Itwangi, ili zifanye vizuri katika mitihani ya kitaifa.

Amesema Shule ya Msingi Masunula imekuwa ikiongoza kwa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa miaka tisa mfululizo, hali iliyomfanya aone umuhimu wa kuipongeza na kuhamasisha shule nyingine kuiga mfano wake.
“Natamani kuona shule zote za msingi katika Jimbo la Itwangi zinafanya vizuri kama Masunula. ndiyo maana nimewaita Walimu Wakuu, Afisa Elimu, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, Kamati za Shule na Sungusungu wajifunze mbinu zinazotumika hapa,” amesema Azza.

Amesema, pongezi hizo haziendi mikono mitupu, bali anawapatia zawadi za bahasha kwa Walimu wote 10 wa shule hiyo, Vikombe vyenye picha ya Mbunge vikiwa na maandishi ya kuwapongeza, na Vikombe pia kwa Serikali ya Kijiji, huku kwa upande wa wanafunzi wote 30 amewapatia “Counter Books” 10 kwa kila mmoja.

Aidha, amesema mbali na pongezi na zawadi hizo, pia changamoto zote ambazo zinaikabili shule hiyo tayari ameshaziwalisha kwa Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe, ambaye pia alipiga simu kwenye hafla hiyo na kuipongeza shule, huku akiahidi kufanya ziara shuleni hapo na kwamba yale yote ambayo Mbunge Azza amemuambia juu ya shule hiyo watayafanyia kazi.
“Shule hii ya Masunula na historia nayo nilishafika hapa mwaka 2017 nikiwa Mbunge wa Vitimaalum, nikiwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga kipindi hicho Jasinta Mboneko na ilikuwa inataka kufungwa sababu ya ukosefu wa choo, nikajenga choo kwa kushirikiana na nguvu za wananchi, hivyo changamoto zote tutazitatua kwa vitendo,”ameongeza.

Pia, amewataka Wazazi, Sungusungu, Serikali ya Kijiji, Kamati ya Shule, Viongozi wa Serikali, waendelee kuwa karibu na Walimu na kuzungumza lugha moja ili waendelee kufaulisha wanafunzi kwa ufaulu wa daraja “A” na kwamba shule zingine zinapaswa kuiga mfano huo wa Masunula.
Ametoa wito pia kwa wanafunzi, kwamba wanapokwenda kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika shule walizopangiwa, wakawe mabalozi wazuri kwa kuitangaza shule hiyo kwa kufanya vizuri zaidi kwenye mithani yao.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela, amempongeza Azza kwa kutoa motisha kwa shule hiyo, pamoja na kuzisemea changamoto za shule hiyo kwa Waziri wa TAMISEM ambaye amezungumza na wananchi kwa njia ya simu na kuahidi kuzitatua kwa vitendo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk. Kalekwa Kasanga, ameipongeza shule hiyo kwa mafanikio ya kitaaluma, huku akiahidi kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini ya changamoto zake ili zitatuliwe.

Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa halmashauri hiyo Andrew Mitumba, amesema Shule ya Msingi Masunula ni jicho la Halmashauri, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi na walimu uendelee.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daudi Shineneko, akisoma taarifa ya shule, amesema ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa na wanafunzi 80, lakini sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 615, pamoja na Walimu 10, Walimu Nane ndiyo walioajiriwa na Walimu wawili wa kujitolea.

Amesema shule hiyo, imeanza kufanya vizuri kitika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la 7 kuanzia mwaka 2015 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya miaka 9 sasa, na malengo yao ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa.
Amesema kwa matokea ya Mtihani wa Taifa la Darasa la 7 mwaka 2025, wanafunzi wote 30 wamepata ufaulu wa Daraja “A” na wanafunzi 18 wamchanguliwa kwenda shule maalumu za bweni, na kwamba mafanikio yao makubwa ni ushirikiano kutoka kwa wazazi, kamati ya shule, sungusungu na viongozi wa serikali ya kijiji.

Ametaja mafanikio mengine ni kufundisha kwa bidii pamoja na kufanya mitahini ya majaribio mara kwa mara.

Mmoja wa wanafunzi waliofaulu Sato Salumu, amemshukuru Mbunge Azza kwa msaada wa vifaa vya shule, akisema nidhamu na kusikiliza walimu ndizo siri ya mafanikio yao.

TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela akizungumza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa akizungumza.
Afisa Elimu wa shule za Msingi Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Andrew Mitumba akizungumza.
Diwani wa Kata ya Usule Masanja Sen akizungumza.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Masunula Daudi Shineneko akisoma taarifa ya shule.
Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamadi akitoa zawadi ya Counter Books kwa wanafunzi waliofaulu.
Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad akitoa zawadi kwa Walimu.
Zawadi zikiendelea kutolewa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464