` KAULI YA PAPA LEO NA MTANANGE WA SIASA NDANI YA KANISA KATOLIKI TANZANIA

KAULI YA PAPA LEO NA MTANANGE WA SIASA NDANI YA KANISA KATOLIKI TANZANIA

KATIKA hali inayoweza kutafsiriwa kama pigo takatifu kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia madhabahu kama majukwaa ya kisiasa, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo, ametoa tamko zito linalotikisa misingi ya uongozi wa kiroho duniani kote. 
Papa Leo, kiongozi wa kwanza wa kanisa hilo kutoka nchini Marekani, amelaani vikali tabia ya viongozi wa dini wanaotumia mamlaka na ushawishi wao kuhalalisha migogoro na migawanyiko ndani ya mataifa yao.

Katika ujumbe wake wa kurasa nne uliotolewa Desemba 18, 2025, kuelekea Siku ya Amani Duniani, Papa amekiri kuwepo kwa kile alichokiita "kufuru"—kitendo cha kutumia lugha ya imani katika vita vya kisiasa na kubariki utaifa uliopitiliza unaochochea vurugu.

Kauli hii ya Vatican inakuja wakati muafaka kwa Tanzania, ambapo mwenendo wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) umeanza kuibua maswali mazito juu ya mwelekeo wa taasisi hiyo katika kulinda amani ya nchi.

TEC na Kivuli cha Siasa: Je, ni Maadili au Maslahi?

Kwa muda mrefu, Tanzania imeshuhudia ukaribu usiosemwa kati ya baadhi ya viongozi wa TEC na vyama vya upinzani, hususan CHADEMA. Ukaribu huu umezua maswali iwapo madhabahu bado ni mahali patakatifu pa sala, au yamegeuzwa kuwa ofisi za siri za kupanga mikakati ya kisiasa. 

Wakati taifa likipita katika vipindi vya majaribu ya uchochezi na uasi, jamii imeshangazwa kuona baadhi ya viongozi hawa wakikaa kimya badala ya kukemea uvunjifu wa amani.

Uchambuzi wa mwenendo wa TEC unaonesha kuwa, mara nyingi sauti ya imani imekuwa ikitumiwa kama kilemba cha shinikizo (blackmail) dhidi ya miradi mikubwa ya kitaifa. Badala ya kutoa mwongozo wa kiroho unaojenga, matamshi ya baadhi ya viongozi yamejaa lawama na vitisho vinavyolenga kukwamisha juhudi za maendeleo.
 
Hali hii inaibua hisia kali kuwa kinachopiganiwa si maadili ya jamii, bali ni "bahasha" na maslahi binafsi yaliyofichwa nyuma ya kivuli cha dini.

Kufuru ya Kidini: Maonyo ya Papa Leo kwa Waumini

Papa Leo amekuwa wazi: "Imekuwa jambo la kawaida kuikuta lugha ya imani katika vita vya kisiasa... kuhalalisha vurugu na mapambano." Hii ni onyo tosha kwa waumini wa Tanzania kuanza kuhoji mafundisho yanayoelekea kuchochea chuki dhidi ya serikali iliyopo madarakani. 
Papa amewataka waumini kukanusha kikamilifu mafundisho ya viongozi wa dini wanaotumia kigezo cha uzalendo kupandikiza mbegu ya mgogoro.

Nchini Tanzania, tumeona matukio ambapo viongozi wa dini wanashupalia mambo yaliyojaa siasa, wakijifanya watetezi wa haki, ilhali ukweli unadhihirisha kuwa kuna harufu ya biashara ya kivuli. 
Amani ya Tanzania haiwezi kuuzwa kwa propaganda, na taasisi za dini hazipaswi kugeuzwa kuwa vyombo vya kutafuta "dili" au kutoa shinikizo kwa serikali ili kupata manufaa ya siri.

Tanzania ya Samia: Ukweli Dhidi ya Propaganda

Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imepiga hatua kubwa katika miradi ya kimkakati, kuanzia maji, nishati, hadi bandari ya uvuvi ya Kilwa. Miradi hii ndiyo inayotoa majibu ya kero za wananchi, na si kelele za lawama zinazoratibiwa na watu wenye njaa ya madaraka na wapenda bahasha.

Taifa halihitaji rushwa ya propaganda kutoka kwa viongozi wa dini waliopoteza mwelekeo; taifa linahitaji ukweli na utulivu. Ni lazima kujiuliza: TEC inakuwa sauti ya nani? Je, wanawakilisha waumini maskini wanaonufaika na miradi ya Samia, au wanawakilisha mikataba ya siri na wafadhili wa nje wanaotaka kuiona Tanzania ikiyumba?

Amani ya Tanzania ni nguzo yetu sote. Kama Papa Leo alivyosisitiza, kutumia dini kuhalalisha migogoro ni kumtukana Mungu. 
Ni wakati wa viongozi wa TEC kurejea kwenye misingi ya kiroho na kuacha kujiingiza kwenye mitego ya kisiasa inayotaka kuunguza nchi. Tanzania si uwanja wa majaribio ya vurugu za kidini au kisiasa. 
Tutaendelea kumlinda Rais wetu kama nguzo ya umoja na kupuuza kila sauti inayojifanya ya kiroho ilhali ndani yake imejawa na njaa ya bahasha na maslahi ya wachache.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464