RC MHITA AFANYA ZIARA KUKAGUA ATHARI ZA MVUA MSALALA, AFARIJI WAATHIRIKA.
Na Johnson James, KAHAMA.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amefanya ziara ya dharura katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Wilaya ya Kahama, kukagua na kujionea athari za mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Desemba 12, na kuleta madhara katika maeneo kadhaa ya makazi na miundombinu ya huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mhita ameonyesha kuguswa na hali ya wananchi waliopatwa na madhara mbalimbali, akitoa maelekezo ya haraka kwa viongozi wa halmashauri kuhakikisha kuwa wananchi wote walioumia au kupata majeraha kutokana na athari hizo, wanapatiwa matibabu bure katika vituo vya afya vilivyo karibu.
Akitembelea Kituo cha Afya Mwanase kilichoathiriwa na mvua, Mhe. Mhita ameagiza kituo hicho kutoendelea kutoa huduma za uzazi katika eneo lililoathirika, kutokana na kuwa hatarishi kwa usalama wa akina mama wajawazito. ametaka eneo hilo kufanyiwa ukarabati wa haraka na kuimarishwa kabla ya kuanza kutumika tena.
“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za afya hazikwami lakini pia tunalinda usalama wa wananchi. Eneo ambalo limeshathibitika kuwa na changamoto za kimazingira linapaswa kutumika kwa tahadhari kubwa,” alieleza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Mhita amemuelekeza Mhandisi wa Halmashauri ya Msalala kupitia upya majengo yote ya umma, hususan yale yanayojengwa kwa nguvu za wananchi, kabla hayajaanza kutumika, ili kuhakikisha yanazingatia viwango na usalama unaohitajika.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Bw. Abdulkadir Mfilinge, ameeleza kuwa huduma za afya kwa sasa zimehamishiwa kwenye zahanati ya karibu, huku juhudi za awali za tathmini na maandalizi ya ukarabati zikianza mara moja kwa kushirikiana na wataalamu wa sekta husika.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imesisitiza msimamo wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya athari za majanga ya asili na kuhakikisha utoaji wa huduma za msingi haukwami hata katika mazingira ya dharura.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464






