.jpg)
Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali za Taifa (MECIRA) kimechukua hatua ya kijasiri ya kuwasilisha barua rasmi katika Balozi za Marekani na Kenya nchini, kikizitaka balozi hizo kuacha kuwa "mapokezi" ya taarifa za uongo na uchochezi zinazopelekwa na watu wanaojiita wanaharakati.
Mwenyekiti wa MECIRA, Habibu Mchange, amesema kuwa kundi la watu wachache walioko nje ya nchi na wale waliopo ndani, wamekuwa wakitumia vibaya uhuru wa maoni kuchochea uvunjifu wa amani na ghasia, huku wao wenyewe wakiishi maisha ya anasa (kula bata) kwenye viyoyozi ughaibuni.
Ukweli Lazima Usemwe: Hatutishwi
Mchange amebainisha kuwa ni dhihaka kwa Taifa la Tanzania kuona balozi za kigeni zikigeuzwa kuwa jukwaa la kusikiliza upande mmoja wa watu wenye ajenda za siri za kutaka kuona Watanzania wakiuawa na mali zao kuharibiwa.
"Tumekwenda kwenye balozi hizi kupeleka ukweli. Tanzania siyo nchi ya kuchezewa na hatuwezi kuruhusu watu wanaojificha nyuma ya 'uharakati' kutumia mataifa rafiki kutuvuruga. Kama wao wanajua kupeleka barua za majungu, na sisi tumepeleka barua za ukweli wa mambo yalivyo," alisema Mchange huku akisisitiza kuwa mzalendo haogopi kusema ukweli.
Hoja ya Mange Kimambi na Usalama wa Taifa
Katika hatua nyingine kali, MECIRA imeitaka Serikali ya Marekani kuacha kumlinda mwanaharakati Mange Kimambi na badala yake ishirikiane na Serikali ya Tanzania kurejeshwa nchini.
Mchange amesisitiza kuwa ni lazima Kimambi ajibu tuhuma za kuchochea vurugu zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Amesema haiwezekani mtu akae nchi za watu akichochea ghasia zitakazopelekea Watanzania kuuana, huku yeye akibaki salama.
MECIRA imezikumbusha Balozi za Marekani na Kenya kuzingatia misingi ya kidiplomasia na kuepuka kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania kwa kuegemea upande wa wachochezi.
Kwa Kenya: Wamewakumbusha kuhusu undugu wa kihistoria na ujirani mwema ambao haupaswi kuchafuliwa na ajenda za watu binafsi.
Kwa Marekani: Wamewataka kutoingizwa kwenye mkenge wa kutoa matamko yanayolinda wavunja sheria kwa kisingizio cha uhuru wa maoni.
MECIRA imesema: "Hatutaruhusu rasilimali na amani ya nchi hii idhoofishwe na watu wanaotaka kutumia damu ya Watanzania kama mtaji wa kisiasa. Kama mnaona Tanzania ni 'poa' ya kuchezewa, mjue kuwa wazalendo sasa wameamka na tutapambana kwa hoja na ukweli popote pale, iwe ubalozini au mitaani."
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464