` WITO WA AMANI NA UMOJA: VIONGOZI WA DINI WAIMARISHA MSINGI WA TAIFA

WITO WA AMANI NA UMOJA: VIONGOZI WA DINI WAIMARISHA MSINGI WA TAIFA

 


Kufuatia matukio ya vurugu na misukosuko ya kisiasa iliyolikumba taifa mwishoni mwa mwaka 2025, viongozi wa dini nchini Tanzania wameendelea kuwa chachu na sauti ya busara na faraja, Wamehimiza wananchi wote kurejea katika misingi imara ya imani, heshima, na maelewano ili kulinda na kuendeleza amani na umoja uliokuwa nguzo ya taifa kwa zaidi ya miongo sita.

Askofu Israel Maasa, Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), amesisitiza umuhimu wa kuitekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano (Reconciliation),Ustahimilivu (Resilience),Mageuzi (Reforms) na Kujenga Upya (Rebuilding).

Askofu Maasa ameeleza kuwa falsafa hii ni tiba muafaka kwa majeraha ya kisiasa na kijamii yaliyotokana na uchaguzi. “Si lazima tukubaliane katika kila jambo, lakini tunaweza kukubaliana katika kutokukubaliana kwa amani. Tunahitaji diplomasia zaidi,” aliongeza Askofu Maasa.

Kwa waamini wa dini tofauti, kauli hii imekuwa mwanga wa matumaini. Hekima ya kuketi meza moja, kusikilizana, na kusamehe inajenga imani ya kitaifa.

Viongozi wa dini wanaamini kwamba maombi na msamaha ni dawa sahihi ya kuponya majeraha ya mioyo ambayo siasa peke yake haiwezi kuyaponya.

Akisisitiza umuhimu wa amani, mwanasiasa mkongwe kutoka mkoani Arusha, Modesti Meikoki, alieleza kuwa hakuna sababu ya kuruhusu maandamano au hasira za kisiasa kugawanya taifa. Alisema, “Matukio yaliyotokea yameleta taharuki kwa wapenda amani duniani. Tuna wajibu wa kurejea katika maadili ya Kikristo na Kiislamu yanayohimiza amani, mshikamano, na utii kwa sheria.”

Viongozi wa dini wametoa wito kwa wananchi kurejelea utu na busara katika maamuzi yao ya kila siku. Wamehimiza kuepuka chuki, kulinda lugha yetu mtandaoni, na kuchagua mazungumzo badala ya mabishano. Katika maombi ya kitaifa yaliyofanyika Dodoma mwezi Novemba 2025, kiongozi mmoja wa dini aliwakumbusha waumini kwamba amani haiwezi kujengwa kwa matusi, bali kwa huruma na heshima.

Kama viongozi wa dini wanavyokumbusha, tuendelee kuomba na kufanya kazi kwa amani. Tuendelee kujenga madaraja ya maelewano badala ya kuta za mabishano. Kwa upendo, kwa huruma, na kwa imani, Tanzania itaendelea kusimama kama mfano wa amani barani Afrika. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464