
Tanzania ni nchi changa, yenye nguvu kubwa ya vijana. Wao ndio uti wa mgongo wa taifa, nguvu kazi ya uzalishaji, na chemchemi ya ubunifu. Lakini nguvu hii kubwa inahitaji mwelekeo sahihi, hekima, na maadili ya kizalendo, hasa katika zama hizi za propaganda za kidijitali.
Katika enzi hizi za habari za kasi, vijana wanatumia mitandao ya kijamii kama chombo cha mawasiliano, lakini mitandao hii pia imekuwa uwanja wa chuki, upotoshaji, na ajenda za siri.
Bw. Lugete Mussa, mchambuzi wa siasa na diplomasia, anasema kuwa baadhi ya mataifa yenye maslahi ya kiuchumi na kisiasa hutumia habari potofu kuvuruga umoja wa Watanzania.
“Vijana lazima waamke. Wasiwe sehemu ya ajenda za watu wanaotaka kuumiza taifa lao kwa jina la demokrasia au haki,” alisema Bw. Lugete.
Kauli yake ni wito wa kizalendo kwa vijana kutambua kuwa taifa linajengwa kwa umoja na maelewano, si kwa kugawanyika na hasira.
Wataalamu wa jamii wanaeleza kuwa vijana wengi wanasukumwa na hasira, wivu, au tamaa ya mafanikio ya haraka, hali inayowafanya waamini kila kitu wanachokiona mtandaoni. Huu ni mtego wa fikra unaotengenezwa makusudi na wapotoshaji ili kuvunja imani ya vijana kwa nchi yao.
Kijana kutoka Dodoma, Bw. Hussein Thomas Mwanga, anaakisi mwamko huu mpya. “Mpaka leo siamini kile kilichotokea Oktoba 29. Nilijifunza kuwa amani haihitaji kelele, inahitaji fikra sahihi. Ni jukumu letu vijana kuitetea amani.”
Maneno yake yanatoa nuru kwamba amani haiwezi kudumu bila haki, lakini haki haiwezi kupatikana kwa ghasia. Tunapodai haki, ni lazima tuikumbuke amani kama chombo cha mazungumzo.
Kizazi cha sasa kinapaswa kuelewa kwamba mitandao si mwalimu wa ukweli. Ni kioo kinachoonyesha taswira kulingana na macho ya anayeitazama. Vijana wanapaswa kutumia muda mwingi kujifunza, kuanzisha miradi, na kutafuta maarifa badala ya kushiriki mijadala ya chuki.
Mchambuzi mmoja wa ajira alieleza ukweli mchungu wa vurugu: “Kila kituo cha mafuta kilichochomwa hakikuwa jengo tu lililoungua, bali ni ndoto, ajira, na maisha ya vijana halisi yaliyoteketezwa.”
Wale wanaochochea vurugu mtandaoni mara nyingi hawapo katika uhalisia wa maumivu yanayofuata. Wanatuma ujumbe kutoka umbali salama, lakini vijana wanaowaamini wanajikuta wakipoteza maisha, kazi, na heshima zao.
Uzalendo wa kweli haupimwi kwa maneno makali ya mitandaoni, bali kwa matendo. Vijana wazalendo ni wale wanaoandika ujumbe wa matumaini, wanaolinda heshima ya nchi yao, na wanaochagua utulivu badala ya fujo.
Bw. Lugete aliongeza kuwa kila kijana ana jukumu la kuilinda taswira ya Tanzania, maana heshima ya taifa haijengwi na viongozi pekee, bali na wananchi wenye uelewa na nidhamu ya fikra.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464