` MAHAKAMA YA WILAYA YA SHINYANGA IMEMHUKUMU KIFUNGO CHA MAISHA JELA BW. MACKIGHTY JULIUS (21) MKAZI WA WILAYA YA SHINYANGA

MAHAKAMA YA WILAYA YA SHINYANGA IMEMHUKUMU KIFUNGO CHA MAISHA JELA BW. MACKIGHTY JULIUS (21) MKAZI WA WILAYA YA SHINYANGA

 

Na Mwandishi wetu kutoka Mkoani Shinyanga. 

Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga imemhukumu kifungo cha maisha jela  Bw. Mackighty Julius (21) mkazi wa Manispaa ya Shinyanga kwa kosa la kupatikana na hatia ya kumbaka binti mwenye umri wa miaka 17 ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama mkazi wa eneo la East Mbezi Mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya Wilaya ya Shinyanga Yusuph Zahoro kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 130(2)(e) ametoa hukumu hiyo baada ya kusoma mwenendo wa kesikwa hiyo leo Novemba 12, 2025 katika Mahakama ya wilaya ya Shinyanga amesema kuwa kwa mujibu wa mlalamikaji ambaye ni shahidi wa kwanza, aliibiwa simu na mshtakiwa akiwa na mwenzie maeneo ya Ngokolo mitumbani na katika kuifuatilia mshtakiwa akamtaka aifuate simu hiyo maeneo ya Tambukareli alipofika ndio alipoingiliwa na wanaume hao wawili, mmoja baada ya mwingine.

Aidha hakimu Yusuph Zahoro amesema Kifungu hicho cha sheria namba 130(2)(e) mtu atahesabiwa ametenda kosa la kubaka endapo atafanya tendo la ndoa na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18 iwe kwa ridhaa au bila ridhaa yake, kifungu cha 131(1) kinaeleza adhabu mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka atahukumiwa kifungo cha maisha jela ili iwe funzo kwa watu

Naye Wakili wa serikali Katandukila Kadata kutoka Mahakama ya wilaya ya Shinyanga amesema kuwa kutokana na kosa hilo na ushahidi ulipo mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwa vijana wengine,

Hata hivyo mshtakiwa Bw. Mackighty Julius alipotakiwa kujieleza kwanini asihukumiwe na kupewa adhabu kali amejaribu kujitetea na kumuomba hakimu ampunguzie kwa madai kuwa ana watoto wadogo na mke pamoja na mama yake mzazi ambaye ni mjane kufuatia Baba yake mzazi kufariki dunia.

“Mheshimiwa naomba kupunguziwa adhabu kwani nina familia ya mtoto, mke, mama mzazi pia na bibi yangu wote wananitegemea, mimi ndio kila kitu baba yangu alishafariki na wadogo zangu pia wananitegemea katika matumizi ya nyumbani na shuleni, ‘Naomba nisamehewe mheshimiwa’” amesema Mackighty Julius.


Na kisha hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga Yusuph Zahoro kwa kwa kizingatia kifungu hicho cha sheria namba 130(20(e) amesema mahakama imemtia hatiani Bw. Mackighty Julius (21) mkazi wa Manispaa ya Shinyanga kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu wengeine wenye tabia kama hizo.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464