Edwin Soko awakunbusha wagombea ahadi ziendane na Dira ya Taifa 2050
Mwandishi wetu,MWANZA
Mwandishi wa habari Mwandamizi na mtetezi wa haki za biinadamu Edwin Soko ameweka bayana kuwa, mgombea wa CCM katika nafasi ya urais amejitahidi kugusa dira ya Taifa ya maendeleo 2050 pale anapotoa ahadi kwenye mikutano ya kisiasa inayoendelea.
Soko amesema hayo Leo Jijini Mwanza kuwa, amekuwa akifuatilia kwa umakini mikutano yote ya wagombea wa nafasi ya urais kwa vyama vyote kumi na Saba vilivyosimamisha wagombea kwa nafasi ya urais na kubaini Chama Cha Mapinduzi kupitia mgombea wake Samia Suluhu na Makamu wake Dakatari Emmanuel Nchimbi wamekuwa wakitoa ahadi zinazogusa mwelekeo wa dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
" Ni vizuri wagombea wengine toka vyama vyote vya siasa watambue kuwa dira ya maendeleo ya Taifa sio nyaraka ya Chama Cha Mapinduzi peke yake bali ni nyaraka ya watanzania vikiwemo vyama vyote vya siasa iliyoandaliwa na wataalamu wa Nchi kwa gharama ya Nchi na ndio mwongozo wa Jumla wa sera na mwelekeo wa maendeleo ya Taifa" alisema Soko.
Soko alifafanua kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni mwongozo wa muda mrefu wa maendeleo ya Nchi, unaolenga kuifikisha Tanzania kuwa Taifa la mafanikio, ustawi, usawa na maendeleo jumuishi ifikapo mwaka 2050 hivyo ni muhimu kwa wagombea wakazingatia hilo ili kuepuka kutoa ahadi zisizo na uwiano kati ya mipango na utekelezaji.
Soko ameongeza kuwa, Kwa upande mwingine, ilani za vyama vya siasa kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2025 zimekuwa ni nyaraka za kisiasa na kiutendaji zilizowekwa kwa ajili ya kushawishi wapiga kura juu ya mipango ya vyama hivyo iwapo vitapata madaraka.
Amesema kuwa, Ingawa dira ya maendeleo ni ya muda mrefu na isiyo ya kisiasa moja kwa moja, ilani za vyama zinapaswa kuakisi au kutekeleza malengo ya muda mrefu yaliyoainishwa katika dira hiyo kwa kipindi kifupi cha miaka mitano ya utawala.
Pia Soko amesisitiza kuwa, Mahusiano Kati ya Dira ya Maendeleo 2050 na Ilani za Vyama vya Siasa ni makubwa kwa kuwa,
dira ya Maendeleo 2050 hutoa mwongozo wa jumla wa sera na mwelekeo wa maendeleo ya taifa. Vyama vya siasa hutumia dira hiyo kuandaa ilani zao, ili kuhakikisha kuwa mipango yao inalingana na vipaumbele vya kitaifa.
Ilani za uchaguzi huchukua malengo ya muda mrefu yaliyomo kwenye dira na kuyapanga katika mikakati ya utekelezaji ya muda mfupi (miaka 5), kama vile,Uboreshaji wa elimu na maarifa, jenzi wa uchumi wa viwanda, kuboresha huduma za afya na kuimarisha miundombinu
Haya yote ni maeneo yaliyotajwa pia katika Dira ya Maendeleo.
Soko aliendelea kusema kuwa, vyama vinaposhika madaraka (kama vile CCM kupitia ilani yake ya 2015), vina wajibu wa kuhakikisha kuwa sera na miradi yao haipingani na dira ya taifa. Kwa mfano, ajenda ya Tanzania ya viwanda ambayo ilisisitizwa sana kwenye ilani ya CCM 2015 ilikuwa sehemu ya kutekeleza dhamira ya Dira ya Maendeleo ya muda mrefu.
Pia aliongeza kuwa,dira ya Taifa inasisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi, asasi za kiraia, na jamii kwa ujumla. Ilani nyingi pia ziliakisi hilo kwa kuahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushirikiano baina ya serikali na wadau wengine.
Kupitia ilani, vyama vya siasa vinaweka ahadi ambazo wananchi wanaweza kuzifuatilia na kuzipima. Dira ya Maendeleo. ya Taifa haina mfumo wa utekelezaji moja kwa moja, lakini inategemea ahadi za vyama (kupitia ilani) kuleta matokeo yanayokusudiwa.
Pia Soko ametoa rai kwa wagombea kutumia vizuri fursa wanaposimama majukwaani na kuomba kura wawaeleze watanzania changamoto zao na ahadi za kutatua changamoto hizo na kuacha kuzungumzia mambo yanayoweza kutafsiriwa kama vituko katika jamii.
'Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ilani za vyama vya siasa hazitenganishwi bali zinategemeana. Dira hutoa mwelekeo wa jumla wa taifa, ilani hutoa ahadi na mikakati ya utekelezaji wa muda mfupi. Vyama vinaposhika madaraka, vinapaswa kuhakikisha kuwa mipango yao ya maendeleo inaendana na dira ya kitaifa ili kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo'" Alihitimisha Soko
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464