` SHYEVAWC ILIVYOCHANGIA KUPUNGUZA MAUAJI YA WAZEE SHINYANGA KUPITIA TAPO LA PAMOJA

SHYEVAWC ILIVYOCHANGIA KUPUNGUZA MAUAJI YA WAZEE SHINYANGA KUPITIA TAPO LA PAMOJA

Baadhi ya wadau wa kikosi kazi cha kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Shinyanga.



Eliasenya Nnko Mkurugenzi wa Shirika la WEADO akieleza namna ambavyo wanatekeleza shughuli za kupinga ukatili kwa wazee

Na Stella Herman,SHINYANGA

Tapo la pamoja la Mashirika ya kupinga ukatili wa kijinsia Mkoani Shinyanga kupitia kikosi kazi kilichoundwa imechangia kupunguza matukio ya mauaji ya wazee kwa imani za kishirikina na tamaa ya mali kwa kushirikiana na serikali.

Hayo yamebainishwa na wadau wa kikosi kazi cha kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa maadhimisho ya siku kimataifa ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee ambayo yamefanyika Kitaifa Mkoani Shinyanga walipokuwa wakieleza kazi mbalimbali wanazofanya katika mabanda yao.

Akieleza baadhi ya kazi walizofanya ambazo zimeonesha mafanikio,Mkurugenzi wa Shirika la (WEADO)ambalo linajihusisha na utetezi wa wazee,wanawake na watoto Eliasenya Nnko, amesema elimu ambayo wanaendelea kuitoa kwa jamii imesaidia kuleta mabadiliko.

Amesema wao wanafanya kazi kama timu kupambana na vitendo vyote vya ukatili kwa wazee,wanawake na watoto kwa kuhakikisha kundi hilo linakuwa salama na kukomesha vitendo vyote vya ukatili kwani binadamu wote wanahaki ya kuishi.
John Eddy kutoka kikosi kazi cha kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto SHYEVAWC

Kwa upande wake John Eddy kutoka kikosi kazi cha kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto,amesema kupitia tapo la pamoja wanaendelea kutoa elimu kwenye Jamii kwa kuhusisha makundi mbalimbali hatua ambayo imesaidia kupunguza matukio ya mauaji.

Amesema maadhimisho hayo ni sehemu pia ya kufanya tathimini kuona ni jinsi gani wanaweza kuendelea kuwalinda wazee kwa ushirikiano wa pamoja,ambapo amesema elimu inaendelea kutolewa kwa makundi rika ili kuhakikisha mauaji ya wazee yanabaki kuwa historia na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii,jinsia wanawake na makundi maalum Mwanaidi Ali Khamis amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kwa watu wote watakaobainika kufanya mauaji,ambapo ametaja takwimu za mauaji ya wazee 

Amesema takwimu za mauaji ya vikongwe zinaonesha mwaka 2022 kulikuwa na matukio 130 ya mauaji wanaume wakiwa ni 29 na wanawake 101 yaliyoripotiwa vituo vya polisi,ambapo mwaka 2023 matukio hayo yaliongezeka hadi kufikia 152 huku wanawake ni 116 na wanaume 36 waliouawa na mwaka 2024 yalipungua na kufikia 138.
Wazee wakiwa kwenye maadhimisho
John Shija akieleza namna ambavyo wanafanya kazi ya kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa wazee na makundi mengine
Mwenyekiti wa baraza la wazee Manispaa ya Kahama Laurent Mihayo akieleza changamoto ya mauaji ya wazee pamoja na baadhi ya watoto kushindwa kuwahudumia watoto wao na kuwatelekeza
Maadhimisho yanaendelea

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464