Mauaji ya wazee ukatili usio na huruma unaohitaji kukomeshwa
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Kwa miaka mitatu mfululizo Tanzania imeendelea kushuhudia mauaji ya wazee hasa vikongwe kwa madai ya ushirikina na sababu nyingine zinazotokana na mila potofu.
Takwimu ambazo zimetolewa Juni 15,2025 na Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Khamisi,kwenye Kongamano la kupinga ukatili dhidi ya wazee mkoani Shinyanga,kwamba ndani ya miaka mitatu mfululizo wazee 420 wameuawa.
Wazee kutoka Shinyanga wakiwa wameshika mabango kupinga ukatili.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2022, waliuawa wazee 130, mwaka 2023 walikuwa 152,na mwaka 2024 wameuawa138.
Mwanaidi anasema,kutokana na kuendelea kwa mauaji ya wazee hapa nchini, kwamba Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau mbalimbali, itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya wazee.
Anasema mkakati huo ni wa mwaka 2018/2019-2022/2023, kwamba japo umeisha muda wake, ila bado serikali itaendelea kusimamia mkakati huo, na watajitahidi kuufanyia maboresho ili ulingane na kuendana na mahitaji halisi ya sasa.
Wazee kutoka Shinyanga wakiwa wameshika mabango kupinga ukatili.
“Serikali itaendelea kutekeleza azma yake ya kuhakikisha wazee wanaishi kwa usalama, sababu kundi hili linahitaji kulindwa dhidi ya vitendo na aina yoyote ya ukatili,”anasema Mwanaidi.
Ametaja sababu ambazo husababisha mauaji ya wazee,kuwa ni mila na desturi,Imani potofu,ramlichonganishi,pamoja na watoto kuwatelekeza wazee wao, na kutaka kuwa dhulumu mali zao, na wengine kudiliki hata kuwatoa uhai.
“Natoa wito kwa jamii kuacha kabisa kufanya matendo yanayoashiria ukatili dhidi ya wazee,bali wanapaswa kuwalinda,kuwathamini na kuacha kutekeleza mauaji dhidi yao,”anasema Mwanaidi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, anasema wazee siyo mzigo, bali ni baraka kwa familia na taifa zima, kwamba wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa hekima zao.
Afisa program kutoka Help Age Tanzania Joseph Mbasha,anasema Jamii inayothamini wazee ni yenye uhai na maadili,na kusisitiza wazee walindwe na kutimiziwa mahitaji yao.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anne Makinda,anasema wazee kwa nchi nzima wapo milioni 3.5, kwa mujibu ya Sensa ya mwaka 2022, na kwamba hiyo ni hazina kubwa kwa Taifa, ambayo inapaswa kulindwa na kuchotwa kwa busara zao,na siyo kutekelezwa kwa mauaji dhidi yao.
“Wazee hawa ni hazina ya busara kwa taifa, badala ya kuwaua,tunapaswa kuwahifadhi na kujifunza kutoka kwao ili kujenga jamii yenye mwelekeo wa maendeleo,”anasema Makinda.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,anasema wazee ni Tunu ya Taifa,hivyo wanapaswa kulindwa kwa gharama yoyote ile dhidi ya vitendo vya ukatili.
Anasema katika mkoa huo wa shinyanga kipindi cha nyuma ulishamiri sana kwa mauaji ya wazee, kwa kukatwa mapanga kutokana na Imani potofu za kishirikiana,lakini sasa hivi yamepungua.
“Mauaji ya wazee yamepungua sana hapa Shinyanga na yamebaki kuwa historia kutokana na uhamasishaji wa jamii na hatua za kiusalama zilizowekwa,”anasema Macha.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa David Sendo,anaiomba serikali kudhibiti mauaji ya wazee pamoja na kuwachukulia hatua kali Wanganga wa kienyeji,ambao wamekuwa wakipiga Ramli Chonganishi, na hata kusababisha mauaji ya Wazee kwa Imani potofu za kishirikina.
Anasema mauaji mengi ya wazee hutokea kwenye kipindi cha uchaguzi,wakati wa migogoro ya kugombea mali,ardhi na mipaka, na idadi nyingi ya wazee huuawa na watu wa karibu na familia zao.
Mzee Ntimba Masalagabo mkazi wa Shinyanga Vijijiji,anasema kwamba jamii au familia wamekuwa wakimuona mzee kama mtu baki,na hapaswi kuendelea kuishi,hasa kwa wale wazee wanaomiliki mali nyingi,na ndiyo wengi huuawa ili watoto au ndugu wamiliki mali hizo.
“Familia zetu zimepoteza utu,wazee tunahitaji kulindwa na sio kuonekana kama watu baki,wasiopaswa kuendelea kuishi,”anasema Masalagabo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 14,inasema kila mtu anayo haki ya kuishi, na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.