` DIWANI KISHAPU : INJILI IENDELEE KUHUBIRIWA, NI CHANZO CHA BARAKA KWA TAIFA

DIWANI KISHAPU : INJILI IENDELEE KUHUBIRIWA, NI CHANZO CHA BARAKA KWA TAIFA

 

Diwani wa Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Joel Ndettoson akizungumza umuhimu wa neno la Mungu kwa wanadamu na taifa alipokuwa akifunga mkutano wa injili ulioandaliwa na kanisa la EAGT Maendeleo Mhunze ulioanza Juni 8,2025 katika viwanja vya Mto mdogo Mwasele "B"
Mchungaji na Mwinjilisti.Joshua Ambangile akihubiri kwenye mkutano ulioandaliwa na Kanisa la EAGT maendeleo Mhunze Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga na kufanyika katika viwanja vya mto mdogo Mwasele "B" Juni 2 hadi 8,2025
Mchungaji kiongozi wa kanisa la EAGT maendeleo lililoko Mhunze Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mch. John Kingu akiwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Kanisa hilo na kufanyika katika viwanja vya mto mdogo Mwasele "B" Juni 2 hadi 8,2025
Makamu Askofu wa EAGT Jimbo la Shinyanga na Mchungaji wa kanisa la EAGT Kishapu Yohana Duba akiwa kwenye mkutano wa injili ulioandaliwa na kanisa la EAGT maendeleo Mhunze ulioanza Juni 2 hadi 8,2025 katika viwanja vya mto mdogo Mwasele "B" Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga


Na Sumai Salum – Kishapu

Diwani wa Kata ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Joel Ndettoson ametoa wito kwa madhehebu ya Kikristo kuendelea kuhubiri Injili ya Kristo, akisisitiza kuwa ni chanzo cha uzima na baraka kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe. Ndettoson ameyasema hayo Juni 8, 2025, alipokuwa akifunga rasmi mkutano wa injili wa siku saba ulioandaliwa na Kanisa la EAGT Maendeleo – Mhunze, chini ya Mchungaji kiongozi John Daud Kingu ulifanyika katika viwanja vya Mto Mdogo, Mwasele “B” na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya Kishapu na Mikoa jirani.

"Nalipongeza Kanisa la mahali pamoja kwa kuandaa mkutano huu mkubwa na kwa kuwakaribisha watumishi wa Mungu kutoka mikoa ya Shinyanga, Tabora na Geita tumebarikiwa kwa uimbaji mzuri na mafundisho ya neno la Mungu tunaamini Mji wetu wa Kishapu umepokea baraka na amani zaidi kupitia mkutano huu,” amesema Ndettoson.

Ametoa rai kwa makutano wote walioudhuria mkutano huo kuwa chachu ya mabadiliko kwa jamii kwa kushiriki kupinga maovu na kueneza amani, huku akiwasihi waendelee kuwa mabalozi wa habari njema kwa wengine.

“Mkutano huu usiwe tukio la kupita bali Kila mmoja wetu anapaswa kutoka hapa akiwa amebadilika kiroho na kimwili pia tuendelee kuliombea Taifa letu, viongozi walioko madarakani na pia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba,” ameongeza Mhe. Ndettoson.

Mhubiri wa mkutano huo, Mchungaji Joshua Ambangile kutoka Igunga, Tabora, ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira salama na huru kwa ajili ya kuhubiri Injili.

"Nampongeza Mkuu wa Wilaya, Mhe. Peter Masindi kwa kuthamini huduma za kiroho nitoe wito kwa serikali yetu tunajua ina wataalamu wengi na wazuri lakini yapo mambo ambayo viongozi wa dini tunayo majibu yake hivyo muwe tayari kushirikiana kwa ajili ya kulijenga taifa kiroho na kimwili, kama ilivyoandikwa kwenye Malaki 2:17,” amesema Mchungaji Ambangile.

Mkutano huo wa Injili ulianza Juni 2 hadi Juni 8, 2025, ulipambwa na huduma za uimbaji kutoka kwa kwaya mbalimbali zikiwemo: Paradiso Kwaya kutoka Nkome (Geita), Shalom Kwaya kutoka Igunga (Tabora), Upendo Kwaya, na EMC Kwaya kutoka Mhunze (Kishapu).
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464