CHADEMA WAMEKIMBIA NA MPIRA KWAPANI MECHI YA UCHAGUZI MKUU 2025:AMOSI MAKALA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo (CCM) Taifa Amosi Makala, amesema Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)wamekimbia na mpira kwapani na kukataa kuchezi Mechi ya Uchaguzi Mkuu (2025) kwa kutoa visingizio visivyo na mashiko.
Makala amebainisha hayo leo Mei 23,2025 wakati akizungumza na Wananchi wa Magazo wilayani Kishapu alipowasili mkoani Shinyanga katika ziara ya kuimarisha Chama pamoja kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara.
Amesema kauli ya "No Reforms No Election" yani hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi ni dalili za kushindwa,kwa kuogopa uchaguzi sababu mabadiliko ambayo wanayadai tayari yalishafanyiwa kazi chini ya utawala wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
"Ajenda ya Chadema siyo No Reforms No Election,bali wamechoka wanataka kukimbia na mpira kwapani wameogopa mechi ya uchaguzi 2025," amesema Makala.
Ametaja mabadiliko ambayo yamefanyika ikiwamo kuundwa kwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo lilikuwa ni hitaji la Chadema, pia uchaguzi hautasimamiwa tena na Wakurugenzi waka hakuna tena kupita bila kupingwa bali kutakuwa na kupigiwa kura za ndiyo na hapana.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa huo kwamba wajiandae na uchaguzi sababu utakuwepo kwa mujibu wa Katiba na hakuna mtu wala chama wa kuuzuia sababu ni takwa la Kikatiba kwamba kila baada ya miaka mitano lazima uchaguzi ufanyike.
Amesema kwamba na uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru na amani na kwamba vyama 18 vitashiriki uchaguzi huo kasoro Chadema ambao watakutana nao 2030.
Awali Makala amewashukuru wananchi wa Shinyanga kwa mapokezi makubwa ambayo ameyapata na kwamba hiyo inaonyesha kwamba Shinyanga ni Ngome ya CCM, na hata kwenye uchaguzi Mkuu wa Serikali kuwa Mkoa huo ulifanya vizuri.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo,akizungumza kwenye mapokezi hayo,amesema Jimbo hilo limepiga hatua kubwa kimaendeleo tofauti na miaka ya nyuma ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amesema amekaribisha Makala,na kuahidi kwamba CCM itashinda kwa kishindo mkoani humo katika uchaguzi Mkuu 2025 na itashika namba moja kwa kura nyingi za Rais Samia.