Header Ads Widget

WATOTO WAWILI WA FAMILIA MOJA WAFARIKI MKOANI GEITA KWA UGONJWA USIOJULIKANA

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dk Omar Sukari
 
Salum Maige, Geita.

WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia huku mama yao mzazi na watoto wengine wawili akiwemo wa umri wa mwaka mmjo wakiwa wamelazwa katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Geita kutokana na ugonjwa usiojulikana uliosababisha watu hao kuhara na kutapika.


Waliofariki ni Kelvin Marco(11) na Monderic Marco(3) ambao ni wakazi wa mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu halmashauri ya mji wa Geita na kwamba watoto hao walifariki aprili 19,mwaka huu baada ya kuhara na kutapika mfulilizo.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Uwanja Enos Chelehani amezungumzia tukio hilo amesema hali ya wanafamilia hao kuanza kuhara na kutapika iliwakuta usiku wa aprili 18 na aliyeanza kuonyesha hali hiyo ni mama wa familia hiyo jina linahifadhiwa.

“Baada ya kufika kwenye hiyo familia taarifa zinasema kuwa, mama ndiye aliyeanza kuhara,ambapo akiwa amelala usiku na mumewe alinyanyuka kwenda chooni ,lakini baadaye mwanaume alimfuatilia na kumkuta amelala na akiwa ameishiwa nguvu baada ya kuharisha”, alisema mwenyekiti huyo.

Alifafanua kuwa , baadaye nao watoto walianza kuhara na kutapika mfulizo ndipo walienda katika zahanati binafisi ya St.Peter ambako waliruhusiwa kurudi nyumbani.

“Wakiwa nyumbani mtoto mmoja akafariki dunia na mwingine naye akawa kwenye hali mbaya pamoja na huyo mama ndipo wakalazimika kwenda hospitali ya mji wa Geita ambako wakiwa wanaendelea na matibabu mtoto mwingine naye akawa amefariki dunia” , ameeleza Chelehani.

Baada ya hali hiyo kutokea mwenyekiti huyo alitoa taarifa kwa viongozi wa juu wa serikali wakiwemo askari polisi kutoka kituo cha Geita ambao walifika nyumbani kwa familia hiyo.

Mmoja wa wahanga wa tukio hilo ambaye amelazwa katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Geita,anasema siku hiyo walikula wali na tunda aina ya tikiti maji,na baadaye wakaenda kulala na ilivyofika usiku wa manane walianza kuhara na kutapika.

“Wale wenzangu waliofariki ndiyo walianza kutapika na kuharisha na kile chakula tulichokula usiku hawa watoto waliofariki hawajakila walikuwa wamelala ,ilivyotokea hiyo hali tukawa tumeletwa huku hospitali na kuanza matibabu,na kwa upande wangu naendelea vizuri”

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omar Sukari amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, waliofariki ni watoto wawili na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya halmashauri ya mji wa Geita.

“Walifikishwa katika Hospitali hii wakiwa wanaharisha na kutapika mlulizo,na sisi kama idara ya afya tunafanya uchunguzi kubaini chanzo cha wao kuharisha na kutapika hadi kupelekea vifo na hawa wagonjwa,tunajua mkoa wetu una tishio la watu kuhara na kutapika,hivyo tumechukua vipimo kujua ni ugonjwa gani”, amesema Dkt.Sukari.

Kuhusu idadi ya waliolazwa Dkt.Sukari amesema, ni mama wa familia hiyo na mtoto wake wa mwaka mmoja pamoja kijana mwenye umri wa miaka 16 ambao hakutaka majina yao yatajwe na kwamba hali zao zinaendelea vizuri na wako chini ya uangalizi maalumu wa watalaamu wa afya.

“Na miili ya hawa watoto tunafanya utaratibu wa kuzikwa na watu watakaohusika kuzika ni watu wetu wa idara ya afya ili kuthibiti hali kama hiyo isijitokeze kwenye familia hiyo na jamii inayozunguka”, amesema Dkt.Sukari.
Post a Comment

0 Comments