Header Ads Widget

MBOZI NA MKAKATI WA MALEZI,MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO


 Mwalimu Ally Njeje akiwa anafundisha darasa lililosheheni zana za kufundishia katika shule ya msingi Shiwinga.

 Na Baraka Messa, Songwe.

Wilaya ya Mbozi  Mkoani Songwe imekuja na mkakati kabambe unaolenga  kufanikisha malengo ya kisera na kimkakati ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto mwenye umri wa miaka kuanzia 0-8 ambao kwa sasa unatekelezwa karibu nchini nzima nchini Tanzania.

 Mkakati huo unaendeshwa na serikali wilayani humo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Save the Children linalofanya kazi zake mkoani Songwe chini ya mradi wa Sida intergrated program kwa kuanzisha mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali na darasa la kwanza lengo likiwa ni kuwaanda vema Ili kumudu kusoma kuandika na kuhesabu kabla ya kuingia madarasa ya juu.

Mratibu wa mradi wa Sida Integrated programme John Tobongo kutoka shirika la Save the Children anasema mafunzo kwa walimu kuhusu utengenezaji zana za kufundishia yamekuwa na manufaa makubwa baada ya walimu 47 kunufaika na kuwa mabalozi kwa walimu wengine katika shule zao.

Anasema pamoja na mafunzo hayo kwa walimu ,pia wametoa mafunzo ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto katika vipengele muhimu vya elimu ya awali, malezi yenye mwitikio , lishe, afya na ulinzi na usalama  wa mtoto.

Anasema mpaka sasa tayari wamezifikia kata 16 katika Wilaya ya Mbozi , ambapo anatanabaisha kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kwa Viongozi wa Kata na vijiji  kwa kuwa wao wapo karibu na Wananchi moja kwa moja hivyo ni rahis kutoa elimu kupitia vikao na mikutano yao.

"Katika mafunzo haya tumejikita katika maeneo muhimu matano ya afua za afya, lishe, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali na Ulinzi na usalama wa mtoto katika miaka miaka 0 mpaka miaka 8, kwa sababu ukuaji wa ubongo wa akili ya binadamu hufanyika kwa kiasi kikubwa" anaeleza Tobongo

 "Kwa  mujibu wa Watalaam wa Sayansi ya Makuzi ya binadamu mtoto anakua kiakili anapokuwa katika umriwa miaka 0-8 na napofikisha miaka 6 ukuaji wa akili kwa maana ya ubongo umbo lake na seli za muunganiko wake vinaimalika kwa asimia 90 , Hivyo kipindi hiki ni muhimu sana katika ujifunzaji wa awali wa mtoto" anaeleza 

Mwezeshaji wa mafunzo ya kutengeneza zana na namna ya kuzitumia Adelina  Kamara anasema watoto wa elimu ya awali katika ujifunzaji wao huhitaji darasa linalongea , ambalo husheheni zana mbalimbali za kujifunzia.

 Kuhusu namna ya kutengeneza zana anasema wamewafundisha walimu kutumia vitu vinavyo wazunguka kama vile, makopo, vijiti, magunzi ya mahindi , mawe na maboksi mbalimbali ambavyo hutumia gharama ndogo.

Anataja faida ya zana za kufundishia kwa watoto kuwa ni ;pamoja na uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi kuongezeka, mwanafunzi kujifunza muda wote hata kama mwalimu hayupo darasani na ujasiri na kujiamini huongezeka kwa watoto.

WALIMU WALIOPATA MAFUNZO WAELEZA 

 Baadhi ya walimu wa madarasa ya awali na darasa la kwanza wilayani Mbozi  waliopata mafunzo ya utengenezaji zana za kufundishia na shirika lisilo la kiserikali la Save the Children

katika Wilaya ya Mbozi wamesema uwepo wa madarasa yanayoongea yaliyosheheni zana zakufundishia yamekuwa kivutio kwa watoto na kupunguza utoro kwa wanafunzi.

Mwalimu wa darasa la awali katika shule ya Msingi Shiwinga Ally Njeje amesema madarasa yenye zana za kufundishia yamekuwa na msaada mkubwa kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza kwa sababu hujifunza kwa vitendo zaidi hali inayowafanya kupenda zaidi kuhudhuria masomo na hata kupunguza kasi ya utoro miongoni mwao.

Alisema awali kabla ya kupata mafunzo ya namna ya utengenezaji zana za kufundishia walimu walikuwa wakitumia nguvu nyingi kufundisha, huku wakiwataka wanafunzi kujifunza kuandika katika umri mdogo.

"Baada ya sera ya elimu na mwongozo wa Serikali 2016 kubadilika na kujumuisha elimu ya awali kuwa ya lazima , kumesaidia kuimalika miundo mbinu ya kufundishia katika madarasa ya awali na darasa la kwanza" amesema Mwalimu Njeje.

Kwa upande wake mwalimu  Martha Mwakasaka kutoka shule ya Msingi Senjele amesema uwepo wa madarasa ya awali na darasa la kwanza yanayoongea ambayo yamesheheni zana za kufundishia yamepunguza utoro kwa wanafunzi kwa sababu wanajifunza kwa kuona ,kushika na kwa kuimba nyimbo.

"Wanafunzi wamekuwa wakifurahia ujifunzaji, muda wote hata kama mwalimu hayupo darasani kwa sababu darasa huvutia na kuwa na picha mbalimbali ambazo hazimchoshi mwanafunzi  anasema Martha.

Kuhusu mafunzo aliyoyapata ya utengenezaji zana za kufundishia  anasema yamemrahisishia katika ufundishaji ,Kwani amekuwa akishirikiana na wazazi wa watoto kutengeneza zana mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yanayo wazunguka. 

Mzazi ambaye mtoto wake anasoma elimu ya awali katika shule ya Msingi Shiwinga Fatuma Makunganya alisema mtoto wake amekuwa na hamasa kubwa ya kwenda shule kutokana na michezo mizuri anayoipata shuleni.

"Mtoto amekuwa akifurahia sana kwenda shule , pia akirudi nyumbani anasimulia na kuelezea picha mbalimbali za wanyama ambazo wanajifunza shuleni, muda mwingine hata siku za mapunziko yaani juma mos na jumapili anauliza kwa nini hawaendi shule" alisema Fatuma.

 Afisa Elimu shule za Msingi na awali katika Wilaya ya Mbozi Dorothy Mwandila amesema mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuimalika kwa miundo mbinu ya madarasa ya awali katika shule zote za Msingi katika Wilaya hiyo.

Amesema pia kumekuwa ongezeko la uandikishaji wa watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza na kuvuka lengo kwa kufikia zaidi ya asilimia  103 katika msimu wa masomo wa mwaka huu wa 2024.

Programu jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto  katika sekta ya elimu inahimiza mazingira rafiki na shawishi kwa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka nane ili kumuwezesha kufurahia mazingira ya shule na kuuwezesha ubongo wake kukua kwa wakatikulingana na umri.

Post a Comment

0 Comments