Header Ads Widget

TAKUKURU SHINYANGA YABAINI URASIMU IDARA YA ARDHI

TAKUKURU SHINYANGA YABAINI URASIMU IDARA YA ARDHI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA.
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga,imebaini kuwapo na urasimu wa utoaji Hati Miliki na Vibali vya ujenzi katika idara ya Ardhi, pamoja na wananchi kutopimiwa maeneo yao kwa wakati licha kulipa pesa.

Hayo yamebainisha leo Aprili 23,2024 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kipindi cha Robo ya Tatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Amesema kwa kipindi hicho TAKUKURU wameweza kubaini kuwapo na Urasimu katika utoaji Hati Miliki na Vibali vya ujenzi, katika Idara ya Ardhi Manispaa ya Kahama.

Amesema pia kupitia program ya TAKUKURU Rafiki walifanya ufuatiliaji wa urasimishaji maeneo ya makazi kwa wananchi wa Kata ya Ndala, ambapo wananchi 246 walichanga kiasi cha Sh. Milioni 12.3 na kulipa Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya kupimiwa ardhi tangu mwaka 2018, lakini hawakuwahi kupimiwa maeneo yao.
Amesema vilevile wananchi wa Mtaa wa Mlepa Manispaa ya Shinyanga wapatao 1,150 nao walishachanga fedha kwa ajili ya kupimiwa na kurasimishiwa maeneo yao tangu mwaka jana, lakini walikuwa bado hawajapatiwa namba za upimaji wa Viwanja vyao.

“Baada ya kupokea kero hiyo, TAKUKURU iliwasilisha Manispaa ya Shinyanga bango kitita lenye kero kusika na mikakati ya utatuzi wa kero hiyo. Halmashauri ya Manispaa Idara ya ardhi walishughulikia kero hiyo ambapo katika mtaa wa Mlepa zoezi la kugawa namba za viwanja lilianza na hadi sasa namba za viwanja 412 zimeanza kugawiwa tangu mwezi Januari na zoezi bado linaendelea”,amesema Kessy.
“Mwezi Februari Manispaa ya Shinyanga ilifanya zoezi la upimaji katika mtaa wa Ndala na kwa sasa Manispaa ipo kwenye mchakato wa ukamilishaji wa utengenezaji wa ramani kwa ajili ya kusajiriwa Wizarani na baada ya hapo kupata namba za viwanja hivyo 246 vya wananchi wa mtaa wa Ndala”,ameongeza.

Aidha, amesema hali hiyo ilikuwa ikisababisha migogoro ya mipaka, kuwanyima fursa ya kupata mikopo katika taasisi za kifedha kwa kutumia ardhi kama dhamana lakini pia viwanja kutoongezeka thamani kwa kukosa utambuzi rasmi.
Katika hatua nyingine amesema walifanya ufuatiliaji kwenye utekelezaji wa Miradi Miwili ya Maendeleo Halmashauri ya wilaya ya Kishapu yenye thamani ya Sh.milioni 224.8, na kubaini Dosari ndogo kwamba katika ujenzi wa Jengo la Utawala Shule ya Sekondari Ukenyenge, walibaini Milango kutengenezwa chini ya kiwango na vigae kutowekewa Grouts.

Mradi mwingine ni ujenzi wa Jengo la ‘One Stop Center’ katika Hospitali ya wilaya ya Kishapu, kwamba Milango Miwili haijafungwa na pamoja na Jengo hilo kutopakwa Rangi ‘Koti’ ya Pili.
Ametoa pia wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kwamba waendelee kutoa taarifa za Rushwa kwenye Ofisi hiyo au wapige simu bure 113, ili zipate kushughulikiwa zikiwamo taarifa za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

Amesema kwa kipindi hicho wamepokea malalamiko 44, ambayo yanahusu Rushwa 20 na uchunguzi wake unaendelea, na yasiyo husu Rushwa ni 24.

Post a Comment

0 Comments