Header Ads Widget

WALIMU 47 ELIMU YA AWALI WANUFAIKA NA MAFUNZO UTUMIAJI ZANA ZA KUFUNDISHIA




 Na Baraka Messa, Songwe.
 
UKOSEFU wa zana za kufundishia katika elimu ya madarasa ya awali na darasa la kwanza katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kumelisukuma shirika lisilo la kiserikali la  Save the Children kutoa mafunzo kwa walimu 47 wanaofundisha elimu ya awali ili kuongeza maarifa ufundushaji.
 
Akiongea na  mwandishi wa BLOG mratibu wa mradi jumuishi kutoka shirika la Save the Children John Tobongo amesema lengo kubwa la mafunzo hayo kwa walimu ni kuboresha msingi wa watoto wa elimu ya awali ili kujifunza vizuri kwa vitendo kupitia vitu mbalimbali vinavyowazunguka.
 
Alisema wameanza na shule 47 ambazo zimetoa mwalimu mmoja mmoja  wa elimu ya awali kila shule kupata mafunzo hayo , ambayo wanaamini yataboresha ujifunzaji wa watoto kupitia kuona na kugusa zana wanazofundishiwa.

" Tumeanzisha mafunzo haya baada ya kubaini kuwa kuna upungufu wa zana za kufundishia katika madarasa ya elimu ya awali, walimu kukosa ujuzi wa kutengeneza zana za kufundishia,

 Lakini pia tumebaini kuwa mtoto anajifunza vizuri zaidi pindi mwalimu anapokuwa na nyenzo za kutosha za kufundishia ambazo hupatikana kulingana na Mazingira yanayowazunguka" alisema Tobongo.

Mwezeshaji wa mafunzo ya kutengeneza zana na namna ya kutuzitumia Adelina  Kamara alisema watoto wa elimu ya awali katika ujifunzaji wao huhitaji darasa linalongea , ambalo husheheni zana mbalimbali za kujifunzia.

 Kuhusu namna ya kutengeneza zana alisema wamewafundisha walimu kutumia vitu vinavyo wazunguka kama vile, makopo, vijiti, magunzi ya mahindi , mawe na maboksi mbalimbali ambavyo hutumia gharama ndogo.

"Mfano rangi ya shilingi 200 au 500 pekee unaweza kutengeneza zana nyingi ambazo zitakuwa na rangi mbalimbali mbazo huwavutia watoto wakati wa kujifunza "  alisema Adelina.

Alitaja faida ya zana za kufundishia kuwa ni ;pamoja na uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi kuongezeka, mwanafunzi kujifunza muda wote hata kama mwalimu hayupo darasani na ujasiri na kujiamini huongezeka kwa watoto.

 Mwalimu wa elimu ya awali kutoka shule ya Msingi Oswe Judith Kamwela alisema wamejifunza namna ya kutengeneza zana kwa gharama ndogo tofauti na awali ambapo walikuwa wanashindwa kutengeneza kwa kuhofia gharama za vifaa vya kutengenezea zana.

 Aliongeza kuwa pia amejifunza namna ya kutengeneza zana kwa kutumia rangi mbalimbali zinazopendezesha darasa ambazo ni rafiki kwa watoto kujifunza.

Kwa upande wake Mratibu wa shule za Msingi na elimu ya awali mkoa wa Songwe Mtinga Maleya alisema toka serikali kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014 kuanzishwa madarasa ya awali yenye miundo mbinu mizuri katika shule zote za Msingi kumepunguza changamoto za watoto kutokujua kusoma na kuandika  kwa kiasi kikubwa.

 Alisema walimu waliopata mafunzo ya namna ya kutengeneza zana  za kufundishia watakuwa mabalozi kwa walimu wengine katika shule zao.



Post a Comment

0 Comments