Header Ads Widget

DARASA LINALOZUNGUMZA NI MBINU NZURI YA MTOTO WA DARASA LA AWALI KUJIFUNZA


Darasa la awali  la mfano katika shule ya msingi Anderson manispaa ya Kahama.

Na Kareny Masasy

PROGRAMU Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) imelenga kuwekeza  moja kwa moja kwenye maendeleo ya binadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija kwa kuhimiza ushiriki wa uchumi ikiwemo sekta ya Elimu.

kupitia program hiyo  inaeleza shule binafsi za madhehebu ya dini mwanzoni  zilionekana kuongoza kutoa elimu ya darasa la awali  nakuwafikia  asilimia tano ya watoto wote wenye umri wa miaka minne  wengi wao wakiwa maeneo ya mjini.

Shule hizo zilikuja na mipango  madhubuti ya kuhakikisha mtoto  anafundishwa  kupitia zana za ujifunzaji zilizo rahisi madarasa  yaliyochorwa  picha  ndani na nje,mikeka ya kupumzikia ikiwemo bembea  kwaajili ya michezo.

 Serikali ya Tanzania imekuja na malengo mahususi ya kuhakikisha wanaanza  kujenga  shule za mfano kwa kuweka dhana na michoro  kupitia mradi wa Boost   kwenye shule chache kwa kila  halmashauri na baadaye kwenye shule zote.

Baadhi ya walimu wanakiri mwanafunzi  wa darasa la awali  anapoona  maneno mafupi  na picha zimechorwa  hupenda kuangalia na  darasa huwa kimya  hata wakiwa peke yao hufundishana.

Mwalimu Christina Gabriel  ambaye ni Mwalimu anayefundisha  darasa la awali shule  ya msingi  Anderson iliyopo kata ya  Majengo manispaa ya Kahama  anasema  darasa  hilo limejengwa mwaka jana (2023) likiwekewa zana zote za ujifunzaji na kuchorwa picha.

“Nilichojifunza kupitia darasa hili watoto  wakiona picha wanakuwa na moyo wa  kujifunza  na kufundishana wao kwa wao kuwa hii ni herufi gani au namba gani”anasema Gabriel.

  mwanzoni walikuwa na darasa ambalo lilikuwa halina dhana za ujifunzaji wala michoro ya picha,michezo ya kwenye bembea nakuwafanya watoto wasitamani kuendelea kuwemo darasani au mazingira ya shule mpaka kutumia nguvu.

“Kutokuwa na darasa lenye dhana za ujifunzaji na dhana za michezo  humfanya mtoto kwanza kuichoka shule mapema kwa kuona hakuna utofauti na nyumbani  lakini sasa hata michoro inawavutia na kubembea”anasema Gabriel.

 Wanafunzi wa  darasa la awali wamekuwa wakifundishwa  mahusiano na kujitambua  kwani  kila mtoto amelelewa katika mazingira yake wanapofika shuleni wanakuwa kitu kimoja cha kuelewana.

 Wanafunzi wa darasa la awali hawatakiwi kuachwa peke yao  muda mrefu kila wakati unakuwa nao  sababu wanatabia tofauti tofauti utakuta mmoja anamchokoza mwingine.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Anderson  Scolastika Leonard  anasema darasa la awali  limejengwa la mfano kupitia mradi wa fedha za  Boost   lina vyumba viwili vya madarasa.

“Kupitia mradi huo  kumejengwa   matundu manne ya vyoo na zana za ujifunza  zilizomo ndani ya madarasa hayo  na bembea za michezo kwa wanafunzi  zilizopo nje ya darasa”anasema Mwalimu Leonard.

Mwalimu Leonard anasema wanafunzi wanaopokelewa kuanza darasa la awali ni  wenye  umri wa kuanzia miaka minne na mitano  ikiwa  maoteo  kwa mwaka 2024 ilikuwa kuwaandikisha  wanafunzi 104 lakini mpaka sasa walioandikishwa ni wanafunzi 131.

Kaimu Ofisa elimu manispaa ya Kahama Sadiki Juma anasema  darasa  la awali  kwa shule ya msingi Anderson   limejengwa mwaka mwaka 2023 kwa gharama ya shilingi Millioni 55 ukijumlisha  matundu ya vyoo manne na  vifaa vyote vinavyohitajika.

Juma anasema kuna shule tatu zilizonjengwa madarasa ya awali ya mfano kupitia  mradi wa Boost  ambazo ni shule ya msingi mlimani, Majengo na Anderson.

“lengo la serikali  kuangalia matokeo ya madarasa hayo na baadaye  zijengwe kwenye shule zote za msingi”anasema Juma.

Ofisa elimu mkoa wa Shinyanga Dafrosa Ndalichako anasema uandikishaji  wa darasa  la kwa mujibu  wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022  matarajio ni kuandikisha  wanafunzi  75,079.

 Mzazi James Kija  mkazi wa kata ya Majengo anasema  mtoto wake ana umri wa miaka mitano   alipomuandikisha  kuanza darasa la awali  alikuwa anakataa kurudi nyumbani  au wakati mwingine anataka kurudi shuleni jioni.

Magreth Samweli mkazi  kata ya  Majengo anasema mtoto wake ana umri wa miaka minne amemuanzisha darasa la awali katika shule hiyo akirudi nyumbani anasimulia picha alizoziona  na alivyobembea.

Mtaalamu wa   Malezi na Makuzi kutoka shirika la Children in Crossfire (CiC)  nchini Tanzania  Davis Gisuka anasema  mtoto akianza kupata  elimu ya awali inamjenge uwezo wa kuanza kufahamu  kuandika na kusoma  na michezo mbalimbali ikiwemo nyimbo.

Kwa mujibu wa toleo la kitabu cha Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi,Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-MMMAM) inaeleza  Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye elimu ya awali kuifanya  kuwa ya lazima.

  Sera ya Elimu na Mafunzo  ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho ni  elimu ya awali katika elimu ya msingi kwa kuzitaka shule zote  za msingi  kuwa na  darasa la elimu ya awali.

Watoto wakichezea bembea

Darasa la mfano



Post a Comment

0 Comments