Header Ads Widget

SERIKALI YAAGIZA ELIMU ITOLEWE KWA WANANCHI CHANJO YA ZIADA (BOOSTER)-UVIKO -19

SERIKALI YAAGIZA ELIMU ITOLEWE KWA WANANCHI CHANJO YA ZIADA(BOOSTER)-UVIKO -19

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akifunga kikao cha tathimini ya Chanjo ya kinga ya Uviko-19.
 Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mulyutu akitoa taarifa ya hali ya chanjo ya Uviko-19 kwa wadau wa afya ambao wameshiriki kikao hicho.

Wakuu wa wilaya za Shinyanga, Johari Samizi (kushoto) na Kahama Mboni Muhita (kulia) wakifuatilia kikao.


Mmoja wa wataalamu kutoka Shirika la THPS, Dkt. Appolinary Bukuku.


Sehemu ya wajumbe wa kikao cha tathimini ya chanjo ya Uviko-19 mkoani Shinyanga wakifuatilia kikao.

Na Suleiman Abeid

HALMASHAURI za wilaya mkoani Shinyanga zimeagizwa kuanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu chanjo ya ziada (booster) kwa watu ambao walichanja chanjo ya kinga ya virusi vya Uviko-19 ili kuimarisha zaidi kinga zao dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme wakati akifungua kikao cha tathimini ya Chanjo ya kinga ya Uviko-19 ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya mkuu wa mkoa.

Kikao hicho kimewakutanisha wakuu wa wilaya, wataalamu kutoka Idara ya Afya ngazi ya mkoa na Halmashauri, wadau wa afya kutoka Shirika la THPS na wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya katika mkoa wa Shinyanga.

Mndeme amesema Serikali kupitia wizara ya afya imepanga kufanyika kwa chanjo ya ziada (booster) kwa wale waliopata chanjo ya awali lengo ikiwa ni kuongeza kinga zaidi kwa walengwa.

Mbali ya halmashauri za wilaya lakini pia Mndeme ameagiza kuwepo kwa ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika kufanikisha chanjo kama ilivyofanyika kwenye chanjo ya awali ambapo mkoa wa Shinyanga ulivuka lengo kwa kuchanja asilimia 100.6.

“Mkoa wa Shinyanga tumefanya vizuri sana katika nchi yetu kwa suala hili la chanjo, tuna kila sababu ya kujipongeza, kwa hiyo tunaamini kinga ni bora kuliko tiba. Lakini pamoja na kufikia lengo la kutoa chanjo hii ya Uviko-19 bado kuna wateja wanaofikia miaka 18 wataendelea kuwepo kila mwaka,”

 

“Serikali kupitia wizara ya afya imepanga kufanyika kwa utoaji wa chanjo ya ziada yaani booster, kwa wale wote waliopata chanjo za awali lengo kuongeza kinga zaidi kwa walengwa, tuendelee kutoa elimu na kushirikisha wadau wote katika zoezi hili,” amesema Mndeme.

Mkuu huyo ameagiza kushirikishwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika zoezi la utoaji chanjo hiyo ya ziada wakiwemo viongozi wa dini, machifu waliopo mkoani Shinyanga, vyombo vya habari, viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji washirikishwe, ili watu wengi waweze kufikiwa.

“Tunataka kila mwananchi ashirikishwe, kwa sababu kulingana na sensa ya mwaka 2022 tunao sasa wananchi wengi na vijana wengi ambao wanaongezeka kuanzia miaka 18 na kuendelea ambao mwaka 2022 hawakuwa katika umri huo, lakini sasa kuanzia mwaka huu wamefikia umri wa miaka 18, wote sasa tuwafikie,” ameeleza.

Hata hivyo mkuu huyo amewataka watendaji wote na wataalamu wa afya wakatoe elimu hiyo kwa kutumia hekima zao badala ya kutumia nguvu na watoe elimu ambayo itawawezesha wananchi kuelewa na waondoe upotoshaji dhidi ya chanjo hiyo ya Uviko-19 inayokwenda kutolewa kwa wananchi.

Wataalamu wametuambia hapa kwamba bado ugonjwa upo, Covid 19 sasa kama bado ipo, sasa tukapate chanjo, twendeni tukatoe chanjo hii na tumwambie mwananchi chanjo hii ni bure na hakuna gharama yoyote, maana Serikali tayari imeishagharimia na tuwaeleze haina madhara kwa mtoto wa kiume wala mtoto wa kike,” amesema Mndeme.

Mndeme amesema walengwa ambao wanakusudiwa kupatiwa chanjo hiyo ya ziada (booster) ni 1,071,395 ambao walipatiwa chanjo za awali na kwamba kwa sababu za ongezeko la umri wa vijana wanaofikia miaka 18 inawezekana malengo hayo yakaongezeka na kufikia watu wengi zaidi.

Amesema zoezi la utoaji wa chanjo hiyo ya ziada linatarajiwa kuanza rasmi Juni 19, 2023 na itakapofika Septemba 30, 2023 walengwa wote wawe wamefikiwa na kupatiwa chanjo hiyo na ofisi yake ipate taarifa ya kazi hiyo Oktoba mosi 2023 na kwamba watakaoshindwa kufikia malengo yaliyowekwa watalazimika kujieleza.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mulyutu amesema mwananchi anapopata chanjo mara nyingi ndivyo anavyoimarisha kinga zake za mwili na kwamba inapotajwa chanjo za booster siyo kwamba ni chanjo mpya.

Chanjo hizi za booster siyo mpya ni zile zile ambazo imelenga kuimarisha kinga ya mwili ya mwananchi, kwa hiyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kuchanja kama walivyojitokeza mara ya kwanza na tukaweza kufikia malengo, na hii ilitusaidia sana kupunguza vifo pamoja na magonjwa yaliyosababishwa na Uviko-19,” amesema Dkt. Mulyutu.

Naye mmoja wa wataalamu kutoka Shirika la THPS ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za kinga kwenye mradi wa afya hatua,  Dkt. Appolinary Bukuku amesema Shirika lake limeamua kushirikiana na uongozi wa Serikali ya mkoa ili aweze kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia viongozi wake.

“Sisi THPS ni miongoni mwa wadau wa masuala ya afya hapa nchini na tumeona namna bora ya kushirikisha jamii juu ya hii chanjo tumeanza na mkuu wa mkoa, tumemwalika hapa amekuja ameongea na wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi ambao ndiyo viongozi wenye watu,”

“Kadri ya maagizo ya mkuu wa mkoa, yatashuka chini kupitia wakuu wa wilaya kwenda kwa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji kama alivyoagiza maana wao ndiyo wenye watu na wataweza kufikisha ujumbe ngazi ya chini, sisi kazi yetu ni kutoa elimu kwa jamii,” Dkt. Appolinary Bukuku.

Amefafanua kuwa shughuli kubwa inayofanywa na shirika lake ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kwamba inapotokea jamii kuwa na mikutano wao hupata nafasi ya kutoa elimu inayohusu umuhimu wa kuchanja chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya  Uviko-19



 

Post a Comment

0 Comments