Header Ads Widget

MLAO ATEMBELEA KITUO CHA WATOTO WENYE ULEMAVU BUHANGIJA ATOA MSAADA NA KUWA MLEZI WAO


Kituo cha watoto wenye ulemavu Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa (NEC) kupitia kundi la vijana Ramadhani Mlao, ametembelea kituo cha kulea watoto wenye ulemavu Buhangija Manispaa ya Shinyanga na kutoa pole kwa kupoteza wenzao watatu mara baada ya mabweni yao mawili kuungua moto, na kutoa msaada wa viti mbalimbali.

Mlao ametembelea kwenye kituo hicho jana akiwa ameambatana na vijana wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga, wakati wakiadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM.

Amesema tukio la mabweni mawili ya watoto hao kuungua moto na kupoteza wenzao watatu, liligusa mioyo ya watu wengi ndiyo maana katika ziara yake hapa mkoani Shinyanga ya kuadhimisha miaka 46 ya CCM, akaona ni vyema apite kituoni hapo na kuwapa pole na faraja, kuwa viongozi wapo pamoja nao.

“Tunawapa pole kwa tukio ambalo lilitokea hapa kituoni kwenu la kuunguliwa moto mabweni yenu mawili na mkapoteza wenzenu watatu, tukio ambalo lilileta simanzi na kugusa mioyo ya watu wengi, sisi kama viongozi na Rais Samia tupo pamoja na ninyi, na kuanzia sasa nitakuwa sehemu ya walezi wa kituo hiki, kwenye shida yoyote nipigieni simu,” amesema Mlao.

Aidha, amesema mbali na kutoa pole pia wametia msaada kidogo wa viti mbalimbali zikiwamo sababu za unga za kufulia. Mafuta ya kujipaka, Juice na Biskuti. 
 
Baadhi ya watoto hao akiwamo John Daima, wameshukuru kutembelewa na viongozi hao wa (UVCCM) na kuwapatia faraja , huku wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mengine, na kumuahidi kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.

Naye Mwalimu Mlezi wa kituo hicho Loyce Daudi ambaye pia ni Mwalimu Mkuu msaidizi katika shule ya Msingi Buhangija, amewashukuru viongozi hao kwa kufika kituoni hapo, na kutaja idadi ya watoto ambao wanao kwa sasa kuwa ni 178, wasioona 18, Viziwi 87 na wenye Ualbino 73.

Aidha, Novemba 23 mwaka jana kulitokea tukio la moto katika kituo hicho cha kulea watoto wenye ulemavu buhangija Manispaa ya Shinyanga na kusababisha watoto watatu wasioona kupoteza maisha huku 31 wakinusurika.

UVCCM, MNEC Mlao, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Anorld Makombe, wakiwa kwenye kituo cha watoto wenye ulemavu Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Msaada wa vitu mbalimbali.

Watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwamo wenye Ualbino ambao wanalelewa katika kituo cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwamo wenye Ualbino ambao wanalelewa katika kituo cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwamo wenye Ualbino ambao wanalelewa katika kituo cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments