Header Ads Widget

KIJANA ANUSURIKA KIFO KWA KUCHARANGWA MAPANGA KICHWANI SHINYANGA AKITOKA KWENYE HARUSI


Baraka Mayala akionyesha majeraha alivyokatwa kichwani kwa mapanga.
Baraka Mayala akionyesha majeraha ya mapanga maeneo ya miguuni.

NA HALIMA KHOYA,SHINYANGA

Baraka Mayala (24) Mkazi wa Burugalila Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga, amenusurika kifo kwa kucharangwa mapanga kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake na watu ambao hawakufahamika wakati akitoka kwenye harusi.

Tukio hilo limetokea Oktoba 7, mwaka huu majira ya saa 4 usiku.

Mayala akisimulia tukio hilo leo amesema watu hao ambao hawafahamu waliokuwa zaidi ya 10 wamvamia njiani wakati akitoka kwenye harusi majira hayo ya saa 4 usiku, na kuanza kumshambulia kwa kumkata mapanga kichwani na sehemu zingine na mwili wake na kisha kumpora kiasi cha fedha Sh. 10,000 na simu ya mkononi.

"Watu hawa walinivamia njiani nikitoka kwenye harusi kuanza kunikagua kwenye mifuko ya suruali na wakati nikijitetea ndipo wakaanga kunishambulia kwa mapanga na wamenikata kichwani mara mbili,na nilipotaka kukimbia walinikata katika miguu yangu, na nilipotaka kutambaa kwa mikono walinikata mikononi kisha wakachukua Sh. 10,000 na simu ya mkononi wakakimbia"amesema Mayala

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dk. Kambi Buteta, alithibitisha kumpokea kijana huyo hoptalini hapo na wanaendelea kumpatia matibabu.

"Tulimpokea Majeruhi kijana Baraka Mayala akiwa na majeraha kichwani, majeraha ambayo yanaashiria alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali, lakini tulifanikiwa kumpatia huduma ya kwanza ili kuzuia damu zisiendelee kuvuja ambapo hali ya kijana huyo ni nzuri kiasi na bado anaendelea kupata matibabu zaidi"amesema Dk, Buteta.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Jackson Mwakagonda, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kubainisha kuwa Jeshi linaendelea na upelelezi.

Post a Comment

0 Comments