Waandishi wa habari nchini wamehimizwa kuzifahamu sheria za habari ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa marekebisho ya sheria hizo unaoendelea hivi sasa.
Rai hiyo imetolewa na mwezeshaji Bw. Jesse Kwayu alipokuwa akiendesha mafunzo ya sheria za habari kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mtwara.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Vyombo vya Habari (IMS) yanalenga kuwajengea uwezo wanahabari mkoani humo kuvifahamu vipengele vya sheria vinavyokandamiza uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa ili waweze kutoa maoni ya kuboresha sheria hizo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Habari na Utafiti wa MISA TAN, Bi. Jacquiline Jones amesema umuhimu wa mafunzo haya unatokana na ukweli kwamba waandishi wa habari ndio wanufaika na wahanga wa sheria hizo.
“Wanahabari ndio wanaozitumia sheria hizi hivyo ni muhimu kuzijua. Hivyo, mafunzo haya ni mahususi katika kuwaongezea uelewa sahihi utakaowasaidia kuzitumia na kubaini changamoto zilizomo na kupendekeza marekebisho yake” alisema Bi. Jones.
Washiriki wa mafunzo hayo walijifunza vipengele mbalimbali vya sheria zikiwemo Sheria ya Huduma za Vvyombo vya Habari, 2016; Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya Mwaka 2016; Sheria ya EPOCA, na Sheria ya Uhalifu wa Mitandaoni, 2015. Pia, washiriki walibadilishana uzoefu hususan utokanao na utekelezaji wa sheria hizo.
0 Comments