Header Ads Widget

LEMBELI ANOGESHA KINYANG’ANYILO CHA KUGOMBEA UENYEKITI CCM MKOA WA SHINYANGA

James Lembeli akiwa ameshika fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
James Lembeli akiwa ameshika fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

James Lembeli ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama kuanzia mwaka (2005-2015) kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, baadae akajiunga CHADEMA na kurudi tena CCM, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti CCM Mkoa wa Shinyanga.


Lembeli amechukua fomu hiyo leo Julai 9, 2022 katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, na kukabidhiwa na Katibu wa Chama hicho Donald Magesa.

Akizungumza wakati wa kuchukua fomu hiyo, amesema ameamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kujipima na kujitathmini na kujiona kuwa nafasi hiyo anaiweza kwa sababu ana uzoefu ndani ya Chama, na pia ni kiongozi mzoefu ndani na nje ya nchi na anaweza kuongoza vizuri Chama.

Lembeli ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira (2010-15),amesema Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, kinahitaji viongozi thabiti, makini na hawana makando kando, sifa ambazo anazo na kuamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti CCM Mkoa.

“Nimejipima na kujitathimini nikaona nije nichukue fomu ili nigombee nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwa sababu sifa zote ni nazo, hasa katika zama hizi ambapo kuna changamoto nyingi,” amesema Lembeli.

Aidha, Julai 6 mwaka huu aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja (2007-2015) kisha akahamia CHADEMA na kurudi tena CCM, naye amechukua fomu ya kugombea tena nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa huo, uchaguzi ambao utafanyika mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa, amesema idadi kamili ya wagombea wote ambao wamechukua fomu ataitaja kesho siku ya hitimisho la uchukuaji fomu.

Post a Comment

0 Comments