Header Ads Widget

WATATU WADAKWA NA MENO YA TEMBO


JESHI la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Kusini, limewakamata watu watatu wakiwa na meno tisa na vipande nane vya meno ya tembo.
 
Kamanda wa polisi mkoani humo, Joseph Konyo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Awadi, Hassan Hakimu na Zakaria Rashid. Alisema watuhumiwa wote wakazi wa Wilaya ya Tunduru walikamatwa Mei 10, mwaka huu katika Kijiji cha Milonde-Kiuma.

Alisema meno hayo yana uzito wa kilo 20.4 na thamani yake ni Sh 138,600,000 na kwamba watuhumiwa watafikishwa mahakamani upelelezi unaoendelea utakapokamilika. Katika hatua nyingine, Kamanda Konyo alisema polisi na askari wa Tawa walifanikiwa pia kukamata meno matano ya tembo yenye uzito wa kilo 44 yakiwa na thamani ya Sh 103,950,000.

Alisema meno hayo yalikamatwa katika Kijiji cha Hanga- Monastery wilayani Namtumbo, baada ya kutelekezwa na watu ambao walistukia mtego uliowekwa na polisi na askari wa Tawa na kukimbia. Alisema jitihada za kuwatafuta ili kuwakamata zinaendelea. Kwa mujibu wa Kamanda Konyo jumla ya tembo saba waliuawa katika matukio hayo mawili na kila tembo mmoja alisema meno yake yana thamani ya Dola za Marekani 1,500.

Alisema kupatikana kwa nyara hizo na kukamatwa kwa watu hao kunatokana na ushirikiano mkubwa kati ya polisi na Tawa. Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Tawa, Kanda ya Kusini Abraham Jullu aliwataka wananchi kuepuka vitendo vya uwindaji haramu wa wanyamapori wakiwamo tembo ambao ni rasilimali na tunu kubwa za taifa.

Alisema uwindaji haramu wanyamapori ni kosa kisheria kwani wanyama hao wanalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuvutia wageni na Watanzania wanaokwenda kutembelea Hifadhi za Taifa na kutoa fedha zinazochangia kukuza uchumi wa nchi yetu. Kamishna Jullu alisema Tawa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitahakikisha vinawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaojihusisha na vitendo vya uwindaji haramu.

Aliitaka jamii kusaidiana na mamlaka husika kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, badala ya wachache kutanguliza maslahi binafsi. Katika hatua nyingine, Kamanda Konyo alieleza kuwa kuanzia Mei Mosi hadi 12, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma lilifanya operesheni maalumu iliyolenga kuwakamata watu wanaojihusisha na matukio ya uvunjaji, wizi na wapokeaji wa mali za wizi katika maeneo mbalimbali.

Alisema katika operesheni hiyo walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 16, wanaume 13 na wanawake watatu wakiwa na vitu vya wizi. Kamanda Konyo alitaja vitu vilivyokamatwa kuwa ni televisheni 10, redio Subwoofer nne, spika moja, magodoro mawili, mitungi mitano ya gesi, viti vya plastiki 10, ndoo 50 za mafuta ya kula, kitanda, mabegi ya nguo na baiskeli moja.

Alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na shughuli za ujangili na matukio ya wizi kuacha mara moja, kwani jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama havitawafumbia macho.

SOMA ZAIDI HAPA CHANZO HABARI LEO.

Post a Comment

0 Comments